MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Fatma Mwassa, ametoa wito kwa viongozi wa dini kuhamasisha jamii umuhimu wa kuhifadhi mazingira.
Kauli hiyo ameizungumza Aprili 29/2023 katika zoezi la upandaji wa miti Bwawa la Mindu Manispaa ya Morogoro lililoandaliwa chini ya uratibu wa Balozi wa Mazingira Ofisi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Chage Alex Chage.
RC Mwassa, amesema kuwa viongozi wa dini wanao wajibu wa kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu kupitia mafundisho ya dini juu ya kutimiza matakwa ya sera ya mazingira ya mwaka 2021 ili malengo yaliyowekwa na serikali katika sekta ya uhifadhi mazingira yanatimia na Tanzania inakuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na mabadiliko ya tabiachi.
Kwa upande Mgeni rasmi katika zoezi hilo la upandaji wa Miti, Askofu wa Kanisa la KKKT-Dayosisi ya Morogoro, Jacob Mameyo , ametumia fursa hiyo kuwasisitiza viongozi wa dini kuhakikisha wanaendelea na utunzaji wa mazingira kwani mazingira yasipotunzwa yanaweza kuleta majanga kama vile ukame,mafuriko na kwamba majanga hayo hayachagui dini bali yanakuja kwa wote.
Naye Mratibu wa Kampeni hiyo ya upandaji wa Miti ambaye pia ni Balozi Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Chege Alex Chage, amesema kuwa suala la Utunzaji wa Mazingira ni Wajibu wa kila Mmoja wetu katika jamii kushirikiana na sekta Binafsi pamoja na Serikali kwa ujumla .
Chage, amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa, kwa usimamizi mkubwa wa utunzaji wa mazingira, pamoja na wadau wote wa Mazingira ambao amekuwa akiungana nao kila anapofanya Kampeni zake ambazo zimekuwa zikitumika kumsaidia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Suleiman Jaffo kwa ajili ya kutimiza wajibu wake.
"Kwa mkoa wetu na Taifa kwa ujumla tumekuwa na kampeni nyingi za Mazingira, tumeanza na wanafunzi kwa kuwa na Kampeni ya Soma na Mti, lakini kwa wananchi nako Ishi na Mti, hizi ni kampeni zenye kulenga uhifadhi wa Mazingira kwa kupanda miti,mimi kwa nfasi ya Ubalozi kazi kubwa ni kumsaidia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Suleiman Jaffo kwa ajili ya kutimiza wajibu wake pamoja na kuona Tanzania yetu tuna rudisha Uoto wa asili katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi" Amesema Chage.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa