VYAMA vya ushirika hapa nchini vimeshauriwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika uendeshaji wa shughuli zake za kila siku ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na kurahisisha kuongeza ufanisi wa kazi katika utendaji wa vyama hivyo.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa Mei 17 mwaka huu wakati akifungua mafunzo ya ya usimamizi kwa Maafisa wa vyama vya ushirika wa kanda ya mashariki inayojumuisha Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro yaliyofanyika katika hoteli ya Savoy Mkoani Morogoro.
Dkt. Mussa amebainisha kuwa ili vyama vya ushirika viweze kujiendesha kibiashara ni wazi suala la TEHAMA kwao halikwepeki na linatakiwa kuwekewa mkazo wa hali ya juu lengo likiwa ni kuondoa dosari ndogo ndogo zinazojitokeza mara kwa mara katika vyama vya Ushirika, hivyo kutojiendesha kibiashsara.
“...tuhakikishe tunatumia ipasavyo tehama, dunia inaendelea na teknolojia inakua kwa kasi, na kwa hakika ikituacha nyuma hakuna kitu kitakachoendelea... kwa hiyo kuna haja ya kuhakikisha kuwa Tume ya maendeleo ya ushirika na vyama vya ushirika vinakuwa na matumizi ya kiwango kikubwa cha Tehama...” amesema Dkt. Mussa.
Akibainisha Changamoto za Vyama hivyo amesema kuna ukosefu wa maadili na uadilifu miongoni mwa viongozi wa vyama hivyo na kushindwa kufikia ndoto waliyo nayo wakulima waliojiunga na vyama vya ushirika.
Katika Hatua nyingine Katibu Tawala huyo ameiagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC)kuhakikisha Tume hiyo inafanya kazi kwa karibu na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuondoa migogoro ya mara kwa mara inayojitokeza kwenye vyama vya Ushirika na kuboresha maisha ya wananchi wa chini ambao ndio walengwa namba moja wa vyama hivyo.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro Ndg. Solomon Kasaba amesema wanatarajia kuona mabadiliko ya uendeshaji wa vyama vya Ushirika na kwamba haitaleta maana kama pamoja na kupata mafunzo hayo bado ushirika utajiendesha kizamani.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Hussein Mohamed amesema ili kufikia Malengo ya Serikali kupitia sekta ya kilimo katika kuchangia fedha za kigeni Bilioni Tano na ajira Bil. Tatu kwa wananchi hasa vijana ifikapo mwaka 2030 ni lazima kuboresha vyama vya ushirika viwe Bora zaidi.
Akielezea faida za vyama vya ushirika Mrajisi na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika TCDC Dkt. Benson Ndiege amesema, mfumo wa kuuza mazao ya kimkakati kupitia vyama vya ushirika una manufaa makubwa tofauti na kuuza mazao hayo kwa mkulima mmoja mmoja.
Akibainisha hayo Dkt. Benson amesema kwa mfano msimu wa kilimo 2021/2022 na 2022/2023 zaidi ya tani trilioni 1.009. za mazao ya kimkakati ikiwemo tumbaku, kahawa, korosho pamba na mkonge ziliuzwa kupitia vyama vya ushirika ambapo zaidi ya Tsh. trilioni 2.9 zilipatikana, kati ya fedha hizo shilingi bilioni 15.144 zilikusanywa kama ushuru kupitia mamlaka za Serikali za mitaa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa