MKUU wa Mkoa wa Morogoro,Mhe.Adam Malima,ametaka waajiri hasa wa Sekta binafsi kuwaruhusu waajiriwa wao ili waweze kujiunga na Chama cha Wafanyakazi chochote ili waweze kunufaika na kuzisaidia sekta zenu kwakuwa ni wajibu na haki kwa pande zote mbili.
Kauli hiyo ameitoa katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani (MEI MOSI) ambayo kwa Mkoa wa Morogoro sherehe zilifanyika katika Uwanja wa Mpira wa miguu wa Jamhuri Morogoro Mei 01-2025.
"Pamoja na kuwapongeza kwa maadhimisho haya leo, nichukue nafasi kuwaelekeza waajiri wote wa Sekta binafsi kuwaruhu watumishi wao kuchagua Chama cha Wafanyakazi chochote na kujiunga kwakuwa ni haki yao nanyi ni wajibu wenu kutekeleza hili," Amesema RC Malima.
RC Malima amewaahidi wafanyakazi wa Mkoa wa Morogoro kuwa yale yote yaliyosemwa na viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Mkoa ameyachukua na kwa yale yaliyo ndani ya uwezo wake atayatekeleza haraka na kwa ufanisi zaidi, na kwa yale yaliyo juu ya mamlaka yake ameahidi kuyafikisha tena kwa maandishi bila kupunguza neno lolote.
Kuhusu suala la Kikokotoo, RC Malima , amesema kuwa ni jambo ambalo kwa hivi karibuni limesemwa na mamlaka mbalimbali na hivyo anayoimani kubwa na Serikali kuwa litafanyiwa kazi na pande zote zitakuwa sawa kabisa kwakuwa Serikali ya Dkt.Samia Suluhu Hassan hii ni sikivu sana.
Aidha,amewataka waajiri kushughulikia haraka mafao ya watumishi wastaafu bila usumbufu huku akiwataka Ofisi ya Kazi Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na OSHA kupeleka majina katika Ofisi yake kwa Taasisi ambazo zinakiuka misingi ya kazi pamoja na usalama wa wafanyakazi kazini.
Katika hatua nyingine,amewataka waajiri kufuata sheria za kuwaajibisha watumishi kwani kutofuata sheria ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na unaweza kuisababishia hasara Serikali.
Pia,ametoa wito kwa waajiri kupeleka fedha za watumishi kwenye mifuko ya hifadhi na kuhakikisha suala la madeni ya watumishi linafanyiwa kazi na yeye Ofisi yake itakuwa mstari wa mbele kufuatilia hilo.
Kauli Mbiu ya Mei Mosi Kitaifa 2025 imebeba ujumbe wa " Uchaguzi Mkuu wa 2025 Utuletee Viongozi Wanaojali na Kuthamini Haki na Maslahi ya Wafanyakazi" Ewe Mfanyakazi Shiriki.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa