Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, mheshimiwa Abdul-Aziz Abood na Mbunge wa Viti Maalum wa jimbo hilo, mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma wamehudhuria na kutoa mapendekezo kwenye kikao maalum cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Morogoro, kilichofanyika tarehe 19.02.2024 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa hiyo, kwa lengo la kujadili bajeti ya Manispaa ya Morogoro.
Mbunge Abood amempongeza Mkuurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa kukamilisha miradi mingi viporo aliyoikuta ndani ya Manispaa miaka miwili iliyopita kisha akashauri uwekezaji zaidi kwenye rasimali watu na vitendea kazi katika sekta ya afya.
“Ndugu Mkurugenzi asante sana kwa ushirikiano wako tumetekeleza ujenzi wa Zahanati na Vituo vya Afya. Sasa tufikirie kuongeza rasilimali watu kwenye maeneo hayo ili wananchi wetu waweze kupata huduma za afya kwa wakati” alieleza mheshimiwa Abood.
Mheshimiwa Ishengoma naye amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa kwa utendaji wake mzuri kisha akamshukuru Rais Samia kwa fedha nyingi za maendeleo ambazo amezileta ndani ya Manispaa ya Morogoro hata kufanikisha miradi mbalimbali kutekelezwa hasa katika sekta za afya na elimu.
Pia, mheshimiwa Ishengoma amesema amefurahi sana kuona jengo dogo la upasuaji (mini-thietre) linajengwa kwenye kituo cha afya cha Sabasaba kwani huduma za upasuaji zitakapoanza kutolewa kituoni hapo itakuwa ni mkombozi kwa wanawake hasa wale wanaopata matatizo wakati wa kujifungua.
“Wanawake wengi wanapenda kujifungulia kwenye kituo cha afya cha Mafiga na SabaSaba hivyo naomba sana ujenzi wa jengo la upasuaji usimamiwe vyema na ukamilishwe haraka” aliongeza kusema mheshimiwa Ishengoma.
Aidha, mheshimiwa Ishengoma ameipongeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa kwa bajeti nzuri iliyowasilishwa na kutoa rai kwamba isimamiwe vyema kusudi Manispaa iweze kukua na hatimaye kukidhi vigezo vya kuwa jiji.
Nao wajumbe wa kikao hicho wakiwemo viongozi wa vyama mbalimbali vya Siasa, na viongozi wa dini wameipongeza ofisi ya Mkurugenzi kwa kuandaa bajeti nzuri kisha wakatoa maoni yao katika sekta za elimu, afya, uchumi, usalama, na miundombinu, maoni ambayo mkurugenzi wa Manispaa, ndugu Ally Machela ameahidi kuyafanyia kazi na kuyaingiza kwenye mpango wa bajeti iliyowasilishwa.
Kwa mujibu wa Mchumi wa Manispaa, ndugu Jeremiah Lubeleje, bajeti ya Manispaa ya mwaka wa fedha 2024/2025 imekisiwa kupanda kwa asilimia 18.8 huku ndani yake kukiwa na miradi 12 ya kimkakati, miradi vipaumbele 18 ya sekta za elimu, afya, utawala, uchumi, ardhi, na miundombinu.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, ndugu Ally Machela ameieleza Kamati hiyo hatua za kimaendeleo ambazo Manispaa imeweza kupiga ndani ya miaka miwili ya uongozi wake, ikiwemo kukamilisha miradi viporo katika sekta za elimu na afya, kujenga Zahanati 10 ambazo saba kati yake yatari zinafanya kazi na tatu zinatazamiwa kuanza kufanya kazi kabla ya mwezi wa sita waka huu, kujenga vituo vya afya Lukobe na Tungi, na kupandisha hadhi Zahanati ya Mazimbu kuwa kituo cha afya.
Hatua nyingine ni kujenga shule nane za Sekondari kwenye kata ambazo hazikuwa na shule hivyo kufanya idadi ya kata zisizokuwa na shule ya sekondari kuwa ni mbili tu kati ya kata zote 29 za Manispaa.
Vilevile, ndugu Machela amesema katika kuboresha sekta ya elimu msingi, Manispaa imejenga shule mbili mpya kwenye kata ya Mindu na Mafisa, na katika ardhi migogoro zaidi ya elfu tatu imetatuliwa, na bajeti ya mapato ya ndani ya Manispaa imepanda kutoka bilioni 10 miaka miwili iliyopita hadi bilioni 16 sawa na ongezeko la bilioni 5.6.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa