Wafanyakazi shiriki wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) mkoa wa Morogoro wamemuomba Rais Dk John Magufuli atupie jicho lake lenye huruma kwenye mifuko ya mafao yanayotolewa na mifuko ya sekta binafsi nchini kwani ni kidogo na kikokotoo cha asilimia 25 inalenga wafanyakazi sekta binafsi.
Kwani mishahara ya wafanyakazi hao ni duni kiasi kwamba , kwa mujibu wa kikikotoo cha asilimia 25 , wastaafu wa sekta hizo , bado watendelea kuumia kwa kulipwa mafao kidogo licha ya usawa katika uchangiaji.
Hayo yalibainishwa katika risala ya wafanyakazi wa TUCTA mkoa wa Morogoro ambayo iliyosomwa na Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Manispaa ya Morogoro , Aboubakar Mpimbi mbele ya Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe.
Mkuu wa mkoa huyo alikuwa mgeni rasmi kupokea maandamano ya amani ya wafanyakazi wa vyama shiriki vya Tucta ya kumpongeza Rais Dk John Magufuli kwa kurejesha kikokotoo cha zamani cha mafao ya wastaafu
. Mpimbi alisema, Tucta mkoa wa Morogoro kwa niaba ya wafanyakazi wote wa mkoa huo wanatoa pongezi zao za dhati kabisa kwa Rais kwa kukubali kupokea kilio cha wafanyakazi cha kulalamikia kikokotoo kipya cha mafao ya kustaafu cha mwaka 2018 na kukisimamisha kwa muda kisitumike kwa sasa.
“ Tunaendelea kumpongeza kwa dhati kabisa kwa kurejesha kanuni ya kikokotoo cha zamani hadi kufikia mwaka 2023” alisema Mpimbi kupitia risala hiyo.
Kupitia risala hiyo alisema , Tucta mkoa wa Morogoro wameendelea kumwomba Rais aendelee kuingilia kati mienendo ya kiutendaji ya mifuko hiyo ili itoe mafao yenye tija kwa wanachama wake na kwa usawa kwa sababu nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuona wanachama wa mifuko wananufaika na mifuko yao.
Akiongea mara baada ya kupokea maandamano hayo Mkuu wa Mkoa Dk Kebwe amewataka wafanyakazi kuiishi na kauli mbiu ya Rais ya “hapa kazi tu” kwa kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na nidhamu ya hali ya Juu.
Hata hivyo aliwataka wafanyakazi wajipange kufanya kazi kwa bidii ili tija iweze kuonekana na kutumia fursa za mikopo inayotolewa na Tasisi za Umma za kifedha kupata mikopo ikiwemo ya mabenki ili iwasaidie kuanzisha miradi ya ujasiriamali na kilimo ili kuendeleza uchumi wao kabla ya kustaafu.
“ Kikokotoo hiki kiwe ni ziada ya kumwezesha mstaafu kuishi vizuri , lakini ukijandaa ukiwa kazini ni jambo jingine la muhimu “ alisema Dk Kebwe.
Katika hatua nyingine aliwaagiza viongozi wa TUCTA mkoa kumpelekea orodha ya taasisi na makampuni yasiyoingiza wafanyakazi wake kujiunga na mifuko ya hifadhi ili aweze kuyachukulia hatua za kisheria kupitia Ofisi ya Waziri mkuu kwani kutofanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi na kuwanyonya wafanyakazi.
Kwa upande wao Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Morogoro Mohamed Simbeye pamoja na Mwenyekiti wa Wanawake cha Chama cha Tpawu mkoa wa Morogoro, Lukia Merey kwa nyakati tofauti walimpongeza Rais kwa kurejesha kikokotoo cha zamani .
Hata hiyo walimwomba pia aendelee kuangalia namna ambayo kikokotoo hicho kutoishia mwaka 2023 bali kiwe endelevu hata baada ya mwaka 2023 na kundi la wafanyakazi wa sekta binafsi kiweze kuongezeka angalao kwa asilimia 40 au 50 sawa na wenzao .
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa