Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mwita Waitara, ameipongeza Manispaa ya Morogoro kwa mipango mizuri na usimamizi mzuri wa usafi huku akitaka nguvu iongezwe katika ufuatiliaji wa upatikanaji wa dampo la Kisasa.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara ya ukaguzi wa dampo la taka Manispaa ya Morogoro lililopo Kata ya Mafisa.
''Nimefurahishwa sana na hatua za kuanza kutekeleza ujenzi wa dampo la Kisasa, mmeniambia tayari andiko lipo na mshaliwasilisha kazi yangu mimi ni kusukuma ili hizo fedha zitoke, lakini niwaombe dampo la kisasa lizingatie miundombinu yote, lisiwe kama hili la kienyeji,mhakikishe mnajiandaa vyema na ujenzi wa dampo Jipya , hili tulilo nalo tuliwekee mazingira rafiki taka zisibaki nje, hapa kuna taka ambazo zinazalisha sumu, haya maji yakitiririka yanawafikia wananchi na ni hatari kwa afya"Alisema Waitara.
Aidha, amesema sio jambo baya Manispaa ikafanya ziara kwa ajili ya mafunzo na kuona wenzenu walivyojipanga katika ujenzi wa madampo pia usafishaji wa Mji .
Mhe. Mwita, amesema kutohudumia dampo hilo ipasavyo kunapelekea uchafuzi wa mazingira, harufu mbaya, na maji yenye sumu kali na kuhatarisha afya ya wakazi wa maeneo jirani viumbe hai na mazingira kwa ujumla.Aidha alisisitiza kuendelea kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kutenganisha taka nyumbani ili waone taka ni dili na sio uchafu mara baada ya kuanzisha kiwanda chenu cha uchakataji wa takataka.
Katika ziara hiyo ameitaka Halmashauri kuwa na mikakati mizuri ya kusimamia usafi ikiwa ni kuwa na mbinu bora za kufanya kila mmoja kuona jukumu la usafi ni lake na kuwa na sheria ambazo zitatekelezwa kwa asilimia mia moja katika usafi ikiwa ni pamoja na tozo za usafi na faini kwa wale waharibifu wa mazingira.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, amesema Wilaya ya Morogoro inakabiliwa na changamoto nyingi za kimazingira lakini wapo tayari sasa kuanza kutekeleza maagizo hivyo watajipanga na timu ya wataalamu kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkoa na NEMC ili kuona changamoto hizo zinafanyiwa kazi.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, amesema wapo katika hatua za kuhakikisha kwamba Kamati zote za Mazingira zinafanya kazi ipasavyo ili kuondokana na tatizo hilo.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba,amesema Manispaa ya Morogoro imetenga bajeti ya shilingi milioni 300 kwa ajili ya ununuzi wa gari la taka ili kuongeza nguvu katika uondoaji wa taka.
Awali akitoa taarifa ya hali ya mazingira na usimamizi wa taka katika Dampo, hilo, Afisa anayesimamia Dampo, Alex Roman, , amemueleza Mhe. Waitara kuwa, Dampo hilo linakabiliana na changamoto mbali mbali ikiwa ni pamoja dampo kutokuwa la kisasa , idadi ya watu wanaongezeka pamoja na uzalishaji wa taka katika Kiwanda cha Mpunga.
Romani, amesema, kwa siku Dampo hilo linapokea tani 180 hadi 200 za taka zinazozalishwa na kuingia katika dampo hilo.
Amesema katika kuhakikisha changamoto hiyo inakwisha, Manispaa ya Morogoro imeandaa eneo Kiegea lenye zaidi ya hekari 1000 ili kujenga Dampo la kisasa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa