Walimu wa shule za Msingi na Sekondari Manispaa ya Morogoro wametakiwa kuzingatia vipindi darasani ili kuweza kuongeza viwango vya ufaulu.
Kauli hiyo imetolewa leo Juni 09,2021 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kilimo na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Dr Tito Kagize, katika hafla ya utoaji wa vyeti na pongezi kwa Waalimu wa Shule za Sekondari Manispaa ya Morogoro waliofaulisha vizuri masomo yao katika kidato cha nne na cha sita mwaka 2020.
Akizungumza na Waalimu hao waliombatana na Wakuu wao wa shule , Dr Kagize, amesema ili ufaulu uweze kuongezeka ni lazima kila mwalimu ahakikishe kwamba anazingatia muda sahihi uliopangwa wa kufundisha vipindi darasani pamoja na maandalio sahihi kwa wanafunzi.
Dr Kagize, amesema kuwa baadhi ya waalimu wengi wamekuwa hawazingatii ufundishaji wa vipindi shuleni jambo ambalo linawafanya wanafunzi kushindwa kuendana na masomo darasani na kupelekea kukosekana kwa uwelewa wa pamoja na kuwa nyuma ya masomo .
Aidha, amesema kuwa ni wakati sasa kila mwalimu atimize wajibu wake darasani ili kuweza kuondokana na sifuri na kuongeza viwango vya ufaulu zaidi ya sasa.
"Waalimu hawazingatii vipindi darasani, kuna utafiti tuliwahi kuufanya kipindi cha nyuma tulikuja kugundua kwamba darasani waalimu hawaingii kwa wakati hivyo wanafunzi wanakosa vya kujifunza, na nilichokigundua ni kwamba kuna waalimu kufundisha ni sehemu ya maisha yao na wengine sio sehemu ya maisha yao na hawa ambao sio sehemu ya maisha yao ndio wanaotuangusha katika suala zima la ufaulu, hivyo twendeni tukafundishe watoto wetu vizuri na kutumia taaluma zetu kikamilifu kuepukana na aibu ya sifuri leo mpo wachache mnaopongezwa lakini matarajio yangu ifikapo mwakani mtaongezeka" Amesema Dr Kagize.
Katika hatua nyingine, Dr Kagize, amewataka Wazazi kuwa na muamko wa kuchangia chakula shuleni ikiwemo waalimu kujenga utaratibu mzuri wa namna ya kuona wanafunzi wanapata uji ili waweze kuwa vizuri darasani.
Mwisho amewapongeza waalimu wote waliofaulisha, Afisa Elimu Sekondari na timu yake kwa kazi nzuri wanazofanya za kufuatilia maendeleo ya wanafunzi shuleni na kuongeza viwango vya ufaulu.
Naye Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Morogoro, Dr Janeth Barongo, amewashukuru waalimu waliofaulisha vizuri huku akiwataka waalimu wengine kuongeza kasi ya ufundishaji.
Dr Barongo, amesema fedha hizo zilizotolewa leo kwa waalimu waliofanya vizuri zimetokana na fedha za zawadi walizotakiwa wapatiwe waalimu hodari 2 waliotakiwa kulipwa kila mmoja shilingi 500,000/= ikiwa ni sehemu ya zawadi zao katika siku ya wafanyakazi duniani lakini wameona ni vyema wakawapongeza waalimu waliofanya vizuri kwa ujumla katika masomo yao kama sehemu moja wapo ya kuwatia nguvu na morali ya ufundishaji.
Aidha, amesema kuwa Serikali imekuwa ikiwekeza sana katika elimu hivyo kuna kila sababu ya kuonesha jitihada za ufaulu ili malengo yaliyowekwa na Serikali ya ufaulu wa juu yaweze kutimia.
Kwa upande wa mwalimu kutoka shule ya Sekondari nanenane , Amina Masomo, ameushukuru Uongozi wa Manispaa ya Morogoro chini ya Afisa Elimu wa Sekondari na timu yake kwa kuwapongeza baada ya kufanya vizuri.
Masomo,amesema kuwa zawadi hizo walizopewa ni chachu ya kufanya vizuri zaidi na kuwafanya wengine waweze kuongeza bidii ya kufundisha.
Miongoni mwa zawadi zilizotelewa ni pamoja na vyeti vya shukrani na fedha taslimu shilingi milioni 1,000,000/= ambapo kati ya hizo wamepewa Wakuu wa shule 3 kila mmoja amepata shilingi 100,000/= na waalimu wa kawaida waliofaulisha katika masomo ambapo jumla yao walikuwa 14 kila mmoja amepata shilingi 50,000/=kwa kila mwalimu aliyefanya vizuri katika somo lake.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa