NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , Angelina Mabula amemwagiza Mkurungezi wa Manispaa ya Morogoro, John Mgalula kufuatilia kwa karibu majina ya wamiliki wa ardhi na viwanja wasiojulikana kwenye mfumo wa ukusanyaji wa mapato kielektroniki na wanadaiwa kukwepa kulipa kodi ya ardhi na kuikosesha mapato Serikali.
Naibu Waziri alitoa agizo hilo alipofanya ziara ya siku moja aliyoifanya Oktoba 17, 2017 katika Manispaa ya Morogoro na kutembelea Ofisi za Ardhi Manispaa hiyo ambayo ilikuwa na lengo la kujionea maendeleo ya mfumo wa ukusanyaji kodi ya ardhi kwa njia ya kielektroniki.
Mbali na kuagiza ufuatiliaji wa majina ya wamiliki hao pia alimtaka Mkurugenzi kutoa maelezo ya kina kuhusiana na majina ya wamiliki wa ardhi kutoonekana katika mafaili yao licha ya nyaraka nyingine muhimu kuwemo.
Katika ukaguzi wake na kuangalia mfumo huo, Naibu Waziri huyo alibaini kuwepo kwa mapungufu makubwa ya uhifadhi wa nyaraka , ikiwemo kufichwa kwa baadhi ya majina ya wadaiwa, ambao wanaonekana hawajalipa kodi ya ardhi kwa muda mrefu.
Naibu Waziri alijionea mafaili zaidi ya 300 ambayo majina hayakuingizwa katika mfumo yakisomeka ‘Ndugu Mhusika’ ambao ni wadaiwa sugu waliolimbikiza madeni kuanzia kiasi cha Sh milioni moja hadi kufikia milioni 25.
“ Nimebaini katika ukaguzi wangu kuwa baadhi ya wateja hawajulikani majina na wameandikwa kwenye mafaili yao ‘ Ndugu Mhusika ‘ ni watu wasiojulikana ingawa kwenye mafaili yao kuna nyaraka za vipimo vya ardhi ya viwanja na nyinginezo isipokuwa hawana majina” alishangazwa Naibu Waziri Mabula.
“ Alimwagiza Mkurugeni watu hao wajulikane majina yao na walipe malimbikizo ya kodi ya ardhi kwa mujibu wa sheria na kuhahidi kupita tena muda mfupi ujao kuona iwapo agizo hili limetekelezwa” alisema Naibu Waziri.
Naibu Waziri alisema , sekta ya ardhi imeachiwa kwa wataalamu wa ardhi na kitendo kinachowafanya baadhi ya Wakurugenzi wa halmashauri za miji, wilaya , Manispaa na Majiji kushindwa kufahamu idadi kamili ya viwanja katika maeneo yao na jambo hilo linatoa mwanya wa udanganyifu wa viwanja na kukosesha mapato serikali.
Pamoja na hayo Naibu Waziri huyo alizitaka Halmashauri zote zilizopo mkoani Morogoro kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye sekta ya ardhi na kuweka ya matumizi bora ya ardhi na upimaji wa maeneo ya makazi na mashamba.
Kwa upande wake Ofisa Ardhi Mteule Manispaa ya Morogoro , Matilda Maktavo alisema, baadhi ya maeneo tayari yameanza kufanyiwa uhakiki, kabla ya kuingizwa kwenye mfumo wa kieletroniki, ili kupata taarifa zilizo sahihi za wateja.
Alisema kuwa mapungufu madogo madogo yaliyojitokeza ni wakati wa uhamishaji wa taarifa kutoka mfumo wa zamani kwenda wa Kieletroniki na hali hiyo inafanyiwa kazi .
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro , John Mgalula alimhakikishia Naibu Waziri kuwa kasoro na changamoto zilzojitokeza wakati wa uhamishaji wa nyaraka kuingizwa kwenye mfumo wa kieletroniki zinafanyiwa kazi kwa ukamilifu ili kutimiza lengo ya ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Hata hivyo alisema , Naibu Waziri huyo katika ziara hiyo amewezesha kutoa somo na kufundisha namna ya uendeshaji wa mfumo huo na kutunza nyaraka na kwamba hakuja kumtafuta mchawi bali ni kuelekeza namna ya uboreshaji wa utendaji wa kazi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa