Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro Sheilla Lukuba ametoa siku saba kwa wamiliki wa Hotel na nyumba za kulala wageni kuanza kulipia madeni yao ya ushuru wa nyumba za kulala wageni ambayo wanadaiwa toka mwaka 2018 hadi sasa.
Mkurugenzi Sheilla ametoa agizo hilo wakati wa ukaguzi wa kupitia nyumba hizo za wageni kuangalia kama wanawaorodhesha wageni katika vitabu vya wageni ambavyo ukaguliwa na Manispaa kwaajili ya kulipia ushuru na kuangalia kama wana leseni za kuendesha biashara hiyo.
Katika ukaguzi huo Sheilla aliongozana na timu ya wataalamu na kugundua wafanyabiashara hao wamekuwa wakifanya udanganyifu mkubwa kwa kutowaorodhesha wageni wanaolala katika Hotel na nyumba hizo za wageni na wengine wamekuwa wana vitabu viwiliviwili na hiyo kupelekea Halmashauri kutopata mapato yanayostahili.
"Katika ukaguzi huu nimegundua kuna udanganyifu mkubwa unaofanywa na wafanyabiashara wa nyumba za kulala wageni na suala hili Serikali haikubaliani nalo ata kidogo,kila mteja anayeingia katika nyumba hizo anapaswa kuorodheshwa katika daftari ambalo hutolewa na Halmashauri"Alisema Mkurugenzi Sheilla.
Mkurugenzi Sheilla amewaagiza wamiliki wote wa Hotel na nyumba za kulala wageni kuanza kulipia kodi ya ushuru wa nyumba za kulala wageni kuanzia sasa na kwa wasiofata sheria kuanzia sasa watafikishwa mahakamani kwa kuwa wanakiuka sheria zilizowekwa.
Katika Ukaguzi huo jumla ya nyumba za kulala wageni kumi na saba zilifungiwa kuendelea kufanya biashara hiyo hadi watakapokidhi vigezo na nyumba sita zilibainika kufuata sheria kwa kuwaorodhesha wageni katika daftari la wageni.
Aidha Mkurugenzi sheria ametoa wito kwa wafanyabiashara wengine kuendelea kulipia kodi mbalimbali wanazodaiwa kama kodi ya Huduma,leseni za biashara na ushuru wa nyumba za kulala wageni.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa