Wananchi wa Manispaa ya Morogoro wametakiwa kuanza kutumia mfumo wa anwani za makazi (NaPA) kutambua makazi na huduma mbalimbali zinazopatikana ndani ya Manispaa yao kwani zoezi la uhakiki wa mfumo huo kwa Manispaa ya Morogoro limekamilika na sasa mfumo uko tayari kuweza kutumika.
Hayo yamebainishwa jana, tarehe 18.10.2023, na Mratibu wa Utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi Taifa, Mhandisi Jampyon Mbugi, wakati alipokuwa akizungumza na wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Morogoro kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, ambapo pia alipokea kutoka kwa wadau hao maoni mbalimbali ya uboreshaji wa mfumo huo ikiwemo ombi la kutobadilisha badilisha namba za anwani na kuhakikisha kunakuwa na mfanano wa vibao vya utambuzi hasa pale vinapowekwa na wananchi wenyewe ama Taasisi.
Kwa upande wake kiongozi wa wataalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ndugu Richard Magubila, ameiomba Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kuhakikisha watendaji wa mitaa wote wanapata elimu ya Anwani za Makazi na wanaendelea kusasisha taarifa za anwani hizo kila mara kunapokuwa na mabadiliko ili kuweza kuufanya mfumo wa anwani za makazi kuwa endelevu.
“Sisi kazi yetu ni kusimamia uingizaji na usasishaji wa taarifa lakini uwekaji wa vibao vya nyumba, na nguzo zenye majina ya barabara ni jukumu la wananchi na wadau. Na kwa kufanya hivi wananchi na wadau wa maendeleo mnakuwa mmeshiriki kuipunguzia Serikali gharama za utekelezaji wa zoezi hili ambalo ni muhimu sana katika kuifanya nchi yetu ifikie uchumi wa kidijitali. Pia hivi karibuni wananchi wa Manispaa ya Morogoro mtapokea jumbe za anwani zingine kwa sababu baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa anwani kwenye Manispaa yenu, kumwekuwa na mabadiliko kadha wa kadha” alieleza Magubila.
Naye Mratibu wa Mfumo wa Anwani za Makazi wa Manispaa ya Morogoro, Bi. Jacquiline Mushi, ameipongeza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kutekeleza zoezi la uhakiki wa anwani za makazi na ametoa rai kwa taasisi za umma na zisizo za umma kushirikiana na Manispaa kuweka vibao vya utambuzi wa barabara na Taasisi zao.
Bi. Mushi pia ameutaka umma wa Manispaa ya Morogoro utambue kwamba, Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo imeandaa na inatoa bure vibao vya namba za nyumba za wananchi wake hivyo wananchi wafike kwenye Ofisi za Kata zao ili wachukue vibao vya namba za nyumba zao.
Kwa upande mwingine, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, ndugu Mussa Ali Mussa, ambaye pia ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika kikao kazi hicho, ameagiza ushirikishwaji wa jeshi la polisi katika zoezi utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi kwa kuwa wao ndio wenye dhamana ya ulinzi na usalama wa raia.
Aidha, ndugu Mussa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dakta Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa zoezi la mfumo wa anwani za makazi (NaPA) kwani kupitia mfumo huo, hivi sasa shughuli za biashara, usafirishaji na usafiri, na usalama wa raia na mali zao vitaimarika zaidi nchini.
Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) unaweza kupatikana kwenye simu janja kwa kupakua program ya (NaPA) kwenye play store ama App Store za simu janja.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa