WANANCHI wa mtaa wa Napome Kata ya Chamwino wametakiwa kuongeza bidii katika kulipia huduma ya urasimishaji wa mtaa wao ili waweze kupata hati na kuepuka migogoro ya ardhi.
Rai hiyo imetolewa leo tarehe 18.07.2023 na Afisa Ardhi wa Manispaa ndugu Valency Huruma wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa mtaa huo waliokuwepo kwenye ofisi ya Kata ya Chamwino wakati Kamati ya Mipangomiji na Mazingira ya Manispaa ilipotembelea mtaa huo ili kuona maendeleo ya zoezi la urasimishaji wa mtaa huo.
“Zoezi la urasimishaji lilipewa kipindi cha miaka 10 hadi kukamilika kwake na mwaka huu ndio wa mwisho hivyo tumieni fursa hii ambayo ni kama ofa ambayo serikali imeitoa kwa wananchi wake nchi nzima mkamilishe malipo ili mpate hati zenu” alifafanua Afisa Ardhi Valency.
Naye Mkandarasi wa Kampuni ya Urasimishaji ya Lunda Ardhi Consult inayotekeleza zoezi hilo la Urasimishaji wa Mtaa wa Napome amesema mpaka sasa kila kiwanja cha mtaa huo tayari kina bikoni na ramani za maeneo yote yaliyopimwa zipo lakini changamoto iliyopo ni kwamba wananchi bado wanaendelea kumegeana kiholela maeneo ya viwanja vyao ambayo tayari yamekwisha kurasimishwa na kati ya viwanja 400 vilivyopimwa na kurasimishwa viwanja 100 tu ndio ambavyo mpaka sasa vimekwisha kulipiwa, hali ambayo inapelekea kukwama kwa ukamilishaji wa zoezi lililobaki la kutoa michoro na kuwapatia watu namba za viwanja vyao.
Hivyo Mwenyekiti wa Kamati ya Mipangomiji na Mazingira ya Manispaa, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwembesongo, Mheshimiwa Ally Rashid Kalungwana,akawaasa wananchi wa mtaa wa Napone kuhamasishana wao kwa wao na kuongeza kasi ya kulipia zoezi hilo la urasimishaji wa mtaa wao ili waweze kupata hati na namba za viwanja vyao.
Aidha, wananchi waliohudhuria katika kikao hicho waliomba elimu zaidi kuhusu bikoni ambazo tayari zimekwisha kupandwa katika viwanja vyao na baada ya kupewa elimu hiyo waliridhia kuongeza kasi ya kulipia zoezi hilo hili waweze kupatiwa namba za viwanja na hati zao.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa