Wakazi wa Mkoa wa Morogoro wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kutolea huduma za Afya ili kutambua Afya zao ikiwemo kupima virusi vya Ukimwi wakiwemo wanaume badala ya wao kusubiri majibu kutoka kwa wenza wao pindi wanapokwenda kupima Afya zao.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro , Dk Kebwe Stephen Kebwe oktoba 6 mwaka huu wakati akizindua kampeni ya FURAHA YANGU iliyofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Kiwanja cha ndege iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro .
Kampeni hiyo imelenga kuhamasisha Jamii kutambua Afya zao ikiwa ni pamoja na kupima virusi vya Ukimwi.
Mkuu wa mkoa alitoa wito huo kufuatia taarifa ya upimaji katika kipindi Januari mwaka 2017 hadi Juni 2018 huku ambacho jumla ya wakazi 341,992 pekee Mkoani humo ndio waliojitokeza kupima virusi vya Ukimwi huku idadi ya wanaume 160,219 na wanawake 181,673.
“Ushahidi wa Kisayansi unathibitisha kuwa mmoja kati ya wanandoa au wapenzi anaweza kuwa na virusi vya Ukimwi na mwingine asiwe navyo, kwa hiyo ndugu zangu wanaume tujitokeze kupima virusi vya Ukimwi tusisubiri majibu ya wake zetu” alisema Kebwe.
Katika kuhakikisha kampeni hiyo inaenea Mkoa mzima wa Morogoro alitoa siku 28 kwa Wakuu wote wa Wilaya za Mkoa huo kuhakikisha wanazindua kampeni hiyo katika Wilaya zao na kutoa taarifa ya utekelezaji wake.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Frank Jacob akimkaribisha Mgeni Rasmi amesema licha ya changamoto zilizopo wanashirikiana na wadau mbalimbali kuhamasisha jamii kujitokeza kupima Afya zao.
Awali akisoma risala ya uzinduzi wa kampeni hiyo mbele ya mgeni rasmi, Mratibu wa huduma za Ukimwi ngazi ya jamii Mkoa wa Morogoro , Dk Emmanuel Mihayo alisema , miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo ni pamoja na muitikio mdogo wa wakazi wa Mkoa huo hasa wanaume kujitokeza kupima Afya zao
Pia uchache wa vituo vya kutolea huduma na matunzo kwa wenye virusi vya Ukimwi (CTC) ambapo kwa sasa Mkoa una jumla ya vituo 66 pekee.
Uzinduzi wa kampeni ya FURAHA YANGU Mkoani Morogoro inafanyika ikiwa ni utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya kupima virusi vya UKIMWI iliyozinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Mkoani Dodoma iliyofanyika Juni 19 mwaka huu ikiwa na lengo la kuwafikia wanaume , vijana na akina mama wajawazito ambapo kauli mbiu yake ni PIMA,JITAMBUE, ISHI.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa