Wanawake mkoani Morogoro wamehimizwa kufanya kazi kwa bidii na kuacha kuwategemea kwa asilimia kubwa wanaume zao na badala yake waungane kuanzisha vikundi vya ujasiriamali vikiwemo vya viwanda vidogo ili kuinua uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.
Ofisa ustawi wa Jamii, Sidina Mathias alisema hayo hivi karibuni katika shule ya msingi Azimio iliyopo kata ya Kihonda katika Manispaa , ukiwa ni mwendelezo wa siku ya wanawake duniani ambayo iliandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Maendeleo ya Jamii (HACOCA) kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya kiserikali ya RIGHT TO PLAY.
Alisema kuwa, endapo wanawake wanajitoa kujiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali hasa viwanda vidogo wanaweza kujikwamua kiuchumi wao wenyewe pamoja na taifa kwa ujumla wake .
Mathias pia amewataka wanafunzi shule za msingi kusoma kwa bidii ili waweze kuondokana na masuala ya unyanyasaji wa kijinsia na kujua kuwa kila mtu anahaki sawa kielimu na kiuchumi.
Kwa upande wa elimu kwa mtoto wa kike alisema , kupitia elimu bora inayotolewa shuleni wanapaswa kusoma kwa bidiii ili waweze kufaulu na kuendelea na elimu ya juu itakayowawezesha kuajiriwa na kujiajiri na hatimaye kujikomboa kiuchumi .
“Ili kwenda na sera ya serikali ya Uchumi wa viwanda vijana mkiwemo wa kike nmapaswa msome kwa bidii ili mweze kutimiza ndoto zenu za kujipatia maendeleo endelevu “ alisema Sidina.
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwasihi wanafunzi wa shule za msingi kusoma kwa bidiii na pia kuiasa jamii iondokane na unyasasaji wa kijinsia kwa watoto hususani wa kike .
Naye Kiongozi wa HACOCA, Watson Mwankusye alisema, kupitia matamasha yanayoendeshwa na Mashirika yasiyo ya kiserikali , wanawake wanapata elimu mbalimbali ikiwemo ya namna ya kujikwamua kiuchumi kwa kushiriki kuanzisha viwanda vidogo katika maeneo yao.
Hivyo aliwataka wanawake wajiamini zaidi katika kuhakikisha wanajikomboa na kuondokana na dhana ya mwanamke akiwezeshwa anaweza ambayo inawavunja moyo wakati wao wenyewe wanaweza.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya msingi Azimio `A` Edith Mkude aliwataka wanawake kutumia fursa ya kauli mbiu ya mwaka huu “Kuelekea uchumi wa viwanda, tuimarishe usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake vijijini” kufanya kazi kwa bidii kwa kujiunga na vikundi mbalimbali ili kujikwamua kiuchumi.
Mkude alisema kuwa, zama za mwanamke kukaa nyumbani na kutegemea mume zimepitwa na wakati na sasa kunahitajika ushirikiano baina ya mume na mke katika kujenga uchumi wa pamoja kwa ajili ya maendeleo ya familia na taifa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa