Wanufaika wa TASAF Manispaa ya Morogoro wametakiwa kutumia kwamalengo yaliyokusudiwa fedha inayotolewa kupitia mpango wa kunusuru Kaya masikini unaotekelezwa na mfuko wa maendeleo ya Jamii nchini TASAF.
Rai hiyo imetolewa leo Aprili 06/2021 na Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro , Hilary Sagara, wakati wakizungumza na wanufaika wa mpango huo katika Kata ya Mwembesongo Manispaa ya Morogoro.
Sagara amefanya ziara fupi ya kukagua utaratibu mzima unaotumika wakati wa kugawa fedha hizo na kujionea namna ya wanufaika walivyotoa ushuhuda ni kwa jinsi gani walengwa hao wameweza kubadilisha maisha yao kupitia mpango huo wa kunusuru Kaya masikini.
Amesema kuwa Serikali kupitia TASAF ,imedhamiria kuondoa umasikini wa kipato unaowakabili wananchi wengi nchini na kwamba ili kuunga mkono jitihada za Serikali wananchi ambao ni wanufaika wa mpango huo wanapaswa kutumia fedha hizo kwa kilie kilichokusudiwa.
Amesema kuwa kumekuwa na taarifa kuwa baadhi ya wanufaika wa mpango wa kunusuru Kaya masikini wamekuwa wakitumia fedha hizo vibaya kinyume na malengo yaliyopo huku wengine wakitumia fedha hizo kuongeza wanawake kwa upande wa wanaume na wengine wakitumia kwa ajili ya ulevi jambo ambalo amelipiga marufuku na kuwataka wanaofanya hivyo kuacha mara moja .
Amesema kuwa mpango huo wenye lengo la kupunguza umasikini unatoa fedha hizo kwa ajili ya matumizi ya elimu, afya lakini cha ajabu wananchi wengi mara baada ya kupata fedha hizo wamekuwa wakibadilisha matumizi mazingira ambayo kila siku wamekuwa wakilalamika kuwa fedha hizo hazitoshi.
"Wananchi ni kweli kuwa pesa hazitoshi lakini kwa hiki kidogo mnachokipata ni vyema mkakitumia kwa malengo mazuri mliyojiwekea , haipendezi kuona mtu umepewa pesa ili umpeleke mtoto wako shuleni lakini hufanyi hivyo na badala yake unaenda kutumia kwa ajili ya ulevi, nawahakikishia kwamba Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro tutafanya ukaguzi wa mara kwa mara kuhusu fedha hizi" Amesema Sagara.
Amesema kushindwa kwa baadhi ya wanufaika kuzitumia fedha hizo kwa usahihi ndiko kunakopelekea wananchi kuendelea kuibebesha lawama kila siku Serikali kuwa imekuwa haifanyi kitu chochote cha maana katika kubadilisha pamoja na kuboresha maisha ya Watanzania.
Hata hivyo, amesisistiza kuwa kutoka sasa Kaya ambayo itabainika kutumia fedha wanazopewa kinyume na utaratibu basi upo uwezekano wa kuiondoa ili wapewe wale wenye shida ya pesa ambayo endapo ikitumika vizuri inaweza kubadilisha maisha ya wanufaika.
Naye Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro ambaye pia ni Afisa Maendeleo Manispaa ya Morogoro, Enedy Mwanakatwe, amewataka kila mlengwa kutumia fedha hizo vizuri kwa ajili ya kusaidia familia kwa kuwapeleka watoto shule, kliniki na kujiwekea akiba.
Mwanakatwe amesema kuwa fedha wanazopatiwa wanapaswa kuzitumia kwa ajili ya kuboresha maisha yao na kusonga mbele ili maisha yao yawe tofauti na wakati ambapo walikuwa hawajaanza kupata fedha hizo.
Hata hivyo Mratibu wa TASAF Manispaa ya Morogoro, Feliciana Katemana, amewataka walengwa wa TASAF kutumia fedha wanazopatiwa na Serikali kutoka hapo walipo na kwenda ngazi nyingine ambayo itawawezesha kuwavusha kutoka katika umasikini na kupata maendeleo.
"Mnatakiwa kujipima katika kipindi hiki ambacho mmekuwa mkipatiwa fedha, na kujiuliza fedha mlizopatiwa zimewasaidiaje?, wapo walengwa katika kipindi hicho wameweza kufanya mambo makubwa, ni vema mkajiuliza TASAF itakapomalizika utakuwa umepiga hatua gani? '" Amesema Katemana.
Kwa upande wa mnufaika wa TASAF, Hidaya Ramadhani Juma, amesema kuwa fedha hizo za TASAF zimesaidia kupata uhakika wa chakula cha kuwafanya wapate mlo mara tatu na kufanya maendeleo mengine ya kujipatia kipato.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa