MAAFISA Watendaji wa kata 29 Manispaa ya Morogoro ,wamesaini mkataba wa upangaji, ufuatiliaji na utekelezaji wa shughuli za Lishe kwenye maeneo ya kata zao, huku wakitakiwa kufanya kazi hiyo kwa kuzingatia malengo makuu , viashiria na vigezo vilivyoainishwa kwenye mkataba huo.
Maafisa hao wamesaini mkataba huo baina yao na Mkurugenzi Januari 24/2023 ,katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi Kuu ya Manispaa.
Mkataba huo wa lishe ni hatua ya muendelezo wa uingiaji wa mikataba ya usimamizi wa shughuli za afua za lishe kuanzia ngazi ya Taifa, Mkoa, wilaya na na hatimaye ngazi ya kata na Mitaa .
Akizungumza wakati wa zoezi la utiaji saini mikataba hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro , Fides Likopero, ameweka wazi kuwa, mkataba huo una malengo makuu mawili ikiwa ni kufanikisha suala la kuboresha hali ya lishe na kupunguza athari za utapiamlo na kuhakikisha jamii inashiriki ipasavyo kupanga, kutekeleza na kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa mpango wa halmashauri wa afua za lishe.
Likopero , amesema kuwa kwa kuzingatia malengo hayo Maafisa Watendaji ambao ni wasimamizi wapaswa kufanya kazi hiyo kwa weledi kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa, kulingana na vigezo na viashiria vilivyoanishwa kwenye mikataba .
"Kila mtu anafahamu umuhimu wa afya bora katika maisha ya binadamu na ujenzi wa Taifa, Serikali imewapa jukumu hili muhimu, nendeni mkalitekeleze kwa umakini mkubwa kulingana na makubaliano, kama kuna changamoto tushirikishane kwa wakati ili kwa pamoja tufikie malengo yaliyokusudiwa na serikali". Amesema Likopero.
Naye Afisa Lishe Manispaa ya Morogoro, Jacqueline Mashurano, amefafanua kuwa, Mkataba wa lishe unawataka Maafisa Watendaji wa Kata kuhakikisha wanashirikiana na Maafisa Watendaji wa Mitaa , kufanya kazi hiyo pamoja na kufanya tathmini na kutoa ripoti ya utekelezaji kwa kila mwezi.
"Lishe duni inanikusababisha umasikini katika Taifa kwani hakutakuwa na Jamii inayoweza kujituma kwa kufanya kazi kutoakana na watu wengi kuathiriwa na utapiamlo, viongozi wenzangu tupambane kutokomeza utapiamlo katika maeneo yetu,ili kuwa na watu wenye afya bora"Amesema Mashurano.
Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Mafiga ,kwa niaba ya Watendaji wenzake, amesema watakwenda kufanyia kazi maelekezo yote kama yalivyo malengo yake kwa kuzingatia vigezo na viashiria vilivyoainishwa kwenye mkata, ikiwa ni pamoja na kuifanya agenda ya kudumu kwenye vikao vyote vya kisheria.
Ifahamike kuwa mkataba wa Lishe ni mkakati wa Kitaifa ambao ulisainiwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na kusainiwa na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa