Watendaji wa Kata na Mitaa Manispaa ya Morogoro wamefanya ibada maalumu ya kumuombea aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli .
Ibada hiyo maalumu iliyoongozwa na viongozi wa dini mbalimbali, imefanyika leo Aprili 03/2021 kwenye Ukumbi wa Kilakala Soko Kuu la Chifu Kingaru Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro ambaye pia ni Afisa Tarafa wa Manispaa ya Morogoro, Winfred Kipako, amesema kuwa Hayati Rais. Dkt. John Pombe Magufuli amejenga misingi imara ya uwajibikaji katika utawala bora, na amekuwa mtetezi wa wanyonge katika maeneo mbalimbali aliyopita.
"Tumeshuhudia namna watu wanavyolia juu ya kifo chake, tunapaswa kujifunza namna ya kutumikia wale tuliopewa dhamana ya kuwatumikia katika mambo yao, kikubwa niwaombe sana Watendaji wenzangu tuendelee kujiepusha na matendo ya ukiukwaji wa maadili na kujikumbusha juu ya umuhimu wa kukuza maadili na kuongeza kasi ya kuwatumikia wananchi ili kufikia malengo ya kitaifa na umuhimu wa kuimarisha maadili" Amesema Kipako.
Kipako, amesema kuwa , watu wameguswa na msiba wa Hayati Rais Dkt John Pombe Magufuli, kutokana na mambo mengi aliyoyafanya kwa muda mfupi wa kipindi cha miaka 5 kwenye sekta ya afya sekta ya elimu, maji barabara usafiri pamoja na maendeleo mbalimbali aliyoyafanya .
Aidha, amesema kuwa Tanzania imekuwa na bahati kubwa sana ya miradi mingi ya maendeleo iliyoanzishwa huku akisema imani yake ni kwamba viongozi waliobakia wakiongozwa na Rais wa sasa Mhe. Samia Suluhu Hassan wataifikisha miradi hii katika hatua iliyokuwa imedhamiriwa kufikiwa.
"Watendaji wenzangu huu sio muda wa kujishika tena tayari tumempata Rais mpya mama yetu Samia Suluhu Hassan , Makamu wa Rais Mhe. Philip Mpango, hivyo tukafanye kazi kwa uadilifu wa kiwango cha juu na kuwatumikia Wananchi kwani tunaamini kabisa kila kitu kilichopangwa kitakwenda vizuri kwa sababu mambo ya serikali yanaenda kwa taratibu zake" Ameongeza Kipako.
Akizungumzia swala la kuendelea kufanya ibada kwa ajili ya kumuombea Hayati Magufuli, Mchungaji Thomas Butabile ambaye pia ni Mhe. Diwani wa Kata ya Mafiga , amesema ni vyema kutafakari sisi tuliobaki tumetanguliza nini kwa muumba wetu kila mtu kwa imani yake.
"Kifo ni safari ya wote na kila mtu ataondoka kwa wakati wake, hivyo ni wakati sasa wakushikamana na kujenga upendo wa dhati kwetu sisi tuliobakia ili kuhakikisha kwamba tunatenda yale yaliyomema kwa wananchi wetu na Taifa letu kwa ujumla" Amesema Mchungaji Butabile.
Mch. Butabile, amesema kuwa sasa Taifa limepata Rais mpya Mh. Mama Samia Suluhu Hassani ambaye ni mama mchapakazi, mzalendo mtiifu muadilifu na mtetezi wa wanyonge, hivyo amewaomba Watendaji wa Kata na Mitaa pamoja na Wananchi kuwa na imani na kuendelea kumpa ushirikiano na kubwa ni kuendelea kumuombea kwa Mungu.
"Kazi ya uongozi ni kazi inayohitaji kumtumaini mungu wakati wote, tuendelee kuwapa moyo viongozi wetu na tuendelee kuwaombea kwa mwenyezi Mungu hakuna jambo litakaloshindikana" Ameongeza Mchungaji Butabile.
Naye Sheikh wa Msikiti wa Kingo, Issa Rajabu Issa, amewataka Watendaji , pamoja na Wananchi kuhakikisha wanaishi kwa hofu ya Mwenyezi Mungu huku akisema kuwa wajenga nchi ni mwananchi hivyo amewataka watendaji hao kuwa na ari na bidii ya kujituma ili kufikia malengo waliyojipangia wakiamini kuwa hakuna atakaekuja kujenga Taifa lao bila ya kuanza wao wazalendo na wengine hufuatia .
Mwenyekiti wa Umoja wa Watendaji wa Kata Manispaa ya Morogoro, Bright Sospeter ambaye pia ni Mtendaji wa Kata ya Chamwino, amewataka Watendaji wenzake kuendeleza uaminifu wenye nidhamu na uadilifu katika kutekeleza majukumu ya kazi zao kama Serikali ilivyowaamini kuwakabidhi majukumu hayo.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Maafisa Watendaji wa Kata Manispaa ya Morogoro ambaye pia ni Mtendaji wa Kata ya Kilakala, Amina Saidi, ameomba ushirikiano uzidi kuendelea kwa Watendaji wenzanke ili kuweza kuifikisha Manispaa mbele na kuwaletea wananchi maendeleo.
Naye Katibu wa Umoja wa Watendaji wa Kata Manispaa ya Morogoro ambaye pia ni Mtendaji wa Kata ya Mazimbu, Prisca Mawala, amewataka Wananachi kuendelea kutoa ushirikiano dhidi ya Watendaji wao kwani maendeleo yanakuja endapo kuna ushirikiano wa kutosha baina ya Wananahci pamoja na Viongozi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa