Kikao cha kikazi kati ya watendaji wa mitaa na kitengo cha Lishe cha Manispaa ya Morogoro, kimefanyika leo tarehe 25.03.2024, kwenye ukumbi wa mikutano wa Manispaa hiyo, kwa lengo la kuendelea kuwajengea watendaji wa mitaa uwezo wa usimamizi wa shughuli za Lishe kwenye maeneo yao ya kazi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho ndugu Shaban Dulu, ambaye ni Afisa Utumishi wa Manispaa anayeshughulika na watendaji wa mitaa na kata, amewapongeza watendaji wa mitaa kwa kuendelea kujituma katika utekelezaji wa majukumu yao kisha akawataka watambue kwamba suala la Mkataba wa Lishe ni la kitaifa hivyo kila mmoja wao ahakikishe anasimamia kikamilifu na kwa kiwango kinachotakiwa utekelezaji wake.
“Fahamuni kwamba suala la Lishe liko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala, ambayo sisi watumishi wa umma ndio watekelezaji wake hivyo nendeni mkasimamie kisawasawa Mkataba wa Lishe, na kila robo taarifa zenu za utekelezaji mziwasilishe kwa viongozi husika wa Manispaa” alisisitiza Dulu.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Lishe Manispaa ya Morogoro ndugu Ester Kawishe, amesema kwa mujibu wa takwimu za kitaifa za hali ya Lishe, Mkoa wa Morogoro bado uko juu katika viashiria vya udumavu, ukondefu na ulishaji wa vichanga na watoto wadogo, huku uzito uliozidi kiasi na kiribatumbo vikiendelea kuongezeka siku kwa siku na kusababisha ongezeko la magonjwa yasiyo ambukiza kama vile saratini, kisukari na mashinikizo ya moyo.
“Wastani wa Serikali wa hali ya udumavu ni asilimia 30, sisi Mkoa wa Morogoro tuko asilimia 31.8 kwa upande wa ukondefu wastani wa Serikali ni asilimia 3.3 sisi tuna asilimia 3.9, na kwa upande wa ulishaji wa vichanga na watoto wadogo wastani wa Serikali ni asilimia 70 ifikapo mwaka 2025 sisi mpaka sasa tuna asilimia 64” alifafanua ndugu Kawishe.
Ndugu Kawishe amesema hali mbaya ya Lishe na udumavu kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano ndio sababu kubwa iliyopelekea mwaka 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye kwa wakati huo alikuwa ni Makamu wa Rais, kuagiza uwepo wa Mkataba wa Lishe na kuzitaka Halmashauri za Serikali za Mitaa kusimamia utekelezaji wake kuanzia ngazi ya kijiji/mtaa hadi ngazi ya mkoa na kitaifa kwa ujumla.
Hivyo amewakumbusha watendaji wa mitaa shughuli wanazopaswa kuzisimamia katika kuhakikisha utekelezaji wa Mkataba wa Lishe ambazo ni kubandika kwenye mbao za matangazo za Ofisi zao, taarifa za watoto wenye umri chini ya miaka mitano, kuadhimisha Siku ya Afya na Lishe kama mtaa huku wakihamasisha wanaume kushiriki katika masuala ya Lishe, na kuhakikisha wahudumu wa afya ngazi ya jamii wanatembelea kaya na kutoa elimu ya Lishe, Afya, Maji na usafi wa mazingira.
Shughuli zingine wanazopaswa kufanya ni kushirikiana na watoa huduma za afya ngazi ya jamii kufanya ufuatiliaji wa watoto walio acha matibabu ya utapiamlo, na kushiriki katika zoezi la utoaji wa nyongeza ya Vitamin A kwa watoto wenye umri wa miezi 6 hadi 59.
Aidha, kwa mujibu wa takwimu za kadi ya alama (score card) ya upimaji wa utekelezaji wa Afua za Lishe, Manispaa ya Morogoro inaonekana kufanya vizuri kwenye afua takriban zote ikiweo upatikanaji wa chakula kwenye shule za msingi na za sekondari za Manispaa, ambapo inaonesha takriban shule zote za Manispaa zinatoa huduma ya chakula kwa wanafunzi wake.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa