Jumla ya watoto 39,524 Manispaa ya Morogoro wenye umri wa kuanzia miezi 9 hadi miezi 59 wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya Surua,Rubella na Polio katika zoezi la utoaji wa chanjo litakalofanyika kuanzia tarehe 15 hadi 19 Octoba 2019 nchi nzima.
Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu wa Manispaa Dkt Ikaji Rashid katika kikao cha PHC kilichofanyika tarehe 23/09/2019 kikiwajumuisha wakuu wa idara mbalimbali Manispaa,wataalamu wa afya na wawakilishi wa madhehebu ya dini.
Akizungumza katika mkutano wa Kamati ya Uraghbishi na uhamasishaji wa zoezi hilo alisema kuwa chanjo hiyo ina uwezo wa kuzuia magonjwa hayo mawili ya Surua na Rubela ambayo yana madhara makubwa kwa watoto chini ya miaka mitano.
Aliyataja madhara hayo ambayo yanazuiwa na chanjo hiyo yenye mchanganyiko wa kinga ya surua na Rubela kuwa ni pamoja na matatizo mengi ya kiafya kama ulemavu wa kudumu, upofu, kutosikia, utindio wa ubongo na vifo.
“Magonjwa hayo mawili yana dalili zake zinafanana sana baada ya upimaji wa kitaalam kukaimisha vimelea vyake na unaweza kuwapata watoto wa rika pana zaidi kuanzia tumboni mwa mama hadi kufikia chini ya miaka 15,” alisema Dkt. Rashid.
Alieleza kuwa, hivyo ndiyo sababu kuu iliyoifanya serikali kuzingatia utafiti na uchunguzi huo na kugharamia chanjo ya kudhibiti magonjwa yote mawili kwa pamoja ili kupanua wigo wa kuwalinda watoto wa taifa hili dhidi ya madhara ya ulemavu na vifo.
Dkt Rashid alisitiza washiriki wa kikao hicho kujitoa kuwaelimisha wananchi juu ya utoaji wa chanjo hiyo na kuwaeleza wananchi kuachana na mila potofu na wajitokeze kwa wingi ili watoto waweze kupata chanjo hiyo ili Halmashauri iweze kufikia asilimia 100.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni "Chanjo ni Kinga kwa Pamoja Tuwakinge"
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa