Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wasisitizwa kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na uadilifu na kuhakikisha wanatoa taarifa kwa wakati.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Ole Sanare alipokuwa anazungumza na Watumishi wa Manispaa tarehe 16/10/2019 ikiwa ni ziara ya kujitambulisha kwa kila Halmashauri na kuzungumza na watumishi na kupeana mikakati ya kufanya kazi.
Amewataka watumishi kusimama imara katika kufanya kazi na kutumia weledi wao kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kutatua changamoto mbalimbali kwa wakati.
Aidha Mhe. Sanare aliwakumbusha watumishi wote wa Umma kutumia vema rasilimali za Serikalizilizopo iwe fedha za kutoka Serikali Kuu ama fedha zinazokusanywa na Halmashauri.
Mhe.Sanare ameupongeza uongozi wa Manispaa ya Morogoro kwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika zoezi la uandikishaji wapiga kura na kuweza kufikia asilimia 82 ya uandikishaji.
Aidha alitoa rai kwa watumishi kujiandikisha na kuendelea kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura ili kwa pamoja tuweze kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 24/11/2019.
"Nakupongeza Mkuu wa Wilaya ya Morogoro na kamati ya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri mliyoifanya katika kipindi cha mvua kwa kushughulikia maeneo yote yaliyopata maafa kutokana na mvua hizo"alisema Mhe.Sanare.
Aidha Mhe.Sanare alipongeza kwa matokeo ya darasa la saba na kuagiza kila Halmashauri kujiandaa kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza na kuagiza wanafunzi wote waliofaulu wanapatiwa nafasi.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Pascal Kihanga alimkaribisha Mkuu wa Mkoa na kumuhahidi kumpa ushirikiano katika utendaji kazi na hasa katika usiamizi wa miradi inayotekelezwa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa