Waumini wa dini Kata ya Mazimbu, wamempongeza Diwani wa Kata hiyo , Mhe. Pascal Kihanga, kwa jitihada za kuwasaidia Ndoo pamoja na Sabuni kwa ajili ya kunawia katika mapambano ya kujikinga dhidi ya Virusi vya Ugonjwa wa CORONA.
Wakizungumza kwa yakati tofauti tofauti, kwa upande wa Sheikh wa Msikiti wa Masjid AQSWA, Sheikh Athumani Msoma, amempongeza Mhe. Diwani kwa jitihada zake za kujikinga dhidi ya Ugonjwa wa CORONA.
“Tuna mshukuru sana Mhe. Diwani wetu , Pascal Kihanga, kwa kweli amekuwa karibu sana na sisi katika kila jambo, lakini kikubwa zaidi ameonyesha ni jinsi gani Serikali ilivyokuwa makini na ugonjwa huu kwa kutuletea ndoo hizi na sabuni , tunamuhakikishia kwamba tutazidi kutoa elimu kwa waumini wetu ili kila anayeingia msikitini anawe maji na sabuni lakini kwakuwa utaratibu wetu sisi Waislamu ni kuchukua udhu ,basi bila shaka na elimu hii tutaelewana wote na kuiunga mkono Serikali kwa mapambano dhidi ya Virusi vya Ugonjwa wa CORONA, Serikali imesema tusilete masihala na kweli tunazidi kuliombea Taifa hili lizidi kuwa katika afya njema na Mwnyezi Mungu inshaallah atatuepushia mbali kama wote tutatekeleza taratibu za Wataalamu bila kuingiza imani zetu”Amesema Sheikh Msoma.
Naye Mchungaji wa Kanisa la TGRC Mazimbu Barakuda, Jailos Maloda, amesema kitendo alichokifanya Diwani wa Kata ya Mazimbu kinapaswa kuigwa na kuchukuliwa kama kiongozi aliyejitoa kwa ajili ya Wananchi wake.
“Tunamshukuru sana Mhe. Diwani wetu kwa kuonyesha moyo wa kipekee sana, hatujategemea kama atafanya jambo kama hili, tumeona baadhi ya maeneno yakifanyika lakini katika nyumba zetu za ibada tumekuwa tukijitegemea wenyewe kununua vifaa hivi, niseme kuwa kuungwa mkono na Serikali ni jambo jema sana,Kanisa letu lina milango minne baada ya kuingia ugonjwa huu, tuliamua kutumia milango miwili amabayo ndiyo tuliyokuwa tumeweka ndoo na kuwalazimisha waumini kupita huko , sasa ametuongezea ndoo nyengine tunatarajia ibada yetu ya kesho na kuendelea milango yote itafunguliwa na kupitika”Amesema Mchungaji Maloda.
Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Mazimbu na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesema kuwa, lengo la kusambaza ndoo hizo katika Nyumba za ibada imetokana na maeneo hayo kuwa na watu wengi na elimu ya kujikinga inaweza kusambaa kirahisi.
Amesema katika utafiti wake amegundua kwamba kwenye Nyumba za ibada ndio kuna watu wengi ambapo hiyo ndiyo sababu iliyomsukuma kuelekeza ndoo katika mmaeneo hayo.
Miongoni mwa nyumba za ibada zilizosambaziwa ndoo hizo ni pamoja na Misikiti na Makanisa yote yaliyopo ndani ya Kata ya Mazimbu ikiwa na lengo la kuwasaidia waumini wa dini kujikinga na Virusi vya Ugonjwa wa CORONA.
“Nimeona nianze na Nyumba za ibada, ukinagalia kwa haraka haraka utagundua kwamba huku kuna watu wengi sana ambao wengine wanakwenda kanisani na Misikitini lakini bado ni Wananchi wangu , kama Serikali inavyosema haina dini, nimeona ni vyema nikapitia miskiti yote pamoja na Makanisa yote yaliyopo katika Kata yangu ili kuyapa nguvu na kuyaunga mkono katika mapambano ya vita dhidi ya Ugonjwa wa CORONA, najua wengine walishaanza kuchukua hatua za kujikinga lakini kama Diwani wao ni jambo la faraja sana kuona kwamba nina kuwa bega kwa bega na Wananchi wangu hususani katika nyumba hizi za ibada , raia yangu kwamba hivi vifaa tuvitumie na nyie Viongozi wa dini najua jinsi gani mnavyoguswa na gonjwa hili, endeleeni kutoa elimu kwa waumini wenu hadi pale gonjwa hili litakapoteketea, tuzidishe maombi katika kuliombea Taifa letu na Viongozi wetu wanaopambana kila uchwao katika kujikinga dhidi ya Maambukizi ya Ugonjwa huu wa CORONA”Amesema Mhe. Kihanga.
Aidha, amewataka wananchi kutodharau ushauri wa Wataalamu badala yake waendelee kuchukua jitihada mahususi za kujikinga na Ugonjwa huo hadi pale mambo yatakapo kaa sawa na kama kuna mtu atajigundua ana viashiria vya Ugonjwa huo apige simu kwa wataalamu kama walivyotoa maelekezo ili hatua za awali ziweze kuchukuliwa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kihanga, amesema anatambua yapo maeneo mengi yana shida lakini ameanza na Nyumba za ibada na ataendelea kufanya hivyo katika maeneoe mengine kadri inavyobidi lengo ni kuhakikisha Wananchi wa Kata yake wanakuwa na uelewa mpana sana juu ya kujikinga na Ugonjwa CORONA pamoja na usalama wa afya zao.
Pia hakuishia katika nyumba za ibada pekee, Mhe. Kihanga ameamua kusambaza ndoo hizo kwa Viongozi wote wa Serikali za Mitaa walio katika Kata yeke akidai kuwa wao wamekuwa wakiwahudumia wananchi kila uchwao.
Pia kwa nafasi aliyokuwa nayo ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, amemuunga Mkono Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, kwa kuweka Ndoo moja nje ya Geti la kuingilia katika Ofisi ya Manispaa yenye kuonyesha ndoo hiyo na udhamini wake kama kiongozi wa Manispaa na kujali afaya za Wananchi wake.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa