Wazazi pamoja na jamii Manispaa ya Morogoro wametakiwa kuwatunza watoto wao kwa kufuata maadili mema na kuwapatia huduma zote za kimsingi ili kuweza kuwaandaa watoto hao kuwa raia wema.
Wito huo umetolewa leo juni 16/2021 kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto Afrika 2021 yaliyofanyika katika Viwanja vya mpira wa miguu Shujaa Manispaa ya Morogoro ambapo mgeni rasmi ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro , Mhe. Pascal Kihanga.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Mhe. Kihanga, amesema kuwa Jamii ina wajibu wa kushirikiana na wazazi katika kuwalea watoto na kuondokana na zana ya mtoto ni baba na mama hivyo kila mzazi anawajibu wa kuwalea watoto katika muongozo na kuhakikisha wazazi kuwapeleka watoto kupata elimu.
Kihanga ,amesema kuwa viongozi wanatakiwa kuhakikisha watoto wanaenda shule huku akitaka wenye mamlaka husika kuhakikisha wanawachukulia hatua za kisheria wazazi wote wasiowapeleka watoto wao shule kupata elimu kwani wazazi wasiopenda kuwapeleka watoto wao shule wanawanyima haki zao za kimsingi.
“Maadhimisho haya nimeyafurahia sana pengine Manispaa ya Morogoro itakuwa imefanya vizuri kuliko Manispaa nyingine, lakini pia nimefurahi kuona maonyesho, shughuli za vipaji mbali mbali vya watoto zikiwemo nyimbo, maigizo sarakasi na mashairi, nawapongeza sana kwa wale watoto walioonesha vipaji vyao hususani Bunge letu la Watoto , na natoa wito kwa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuendelea kuvilea, kuviendeleza na kuvikuza vipaji hivi ili baadae watoto pamoja na Taifa letu liweze kunufaika na vipaji hivi” Amesema Mhe. Kihanga.
“Aidha, nimesikia risala ya watoto ambayo imejumuisha haki za kimsingi za watoto ambayo imebainisha wazi changamoto wanazopitia watoto wetu zenye kukatisha ndoto zao lakini pia yenye kutoa majukumu ya kila mdau yaani wazazi/walezi, familia, taasisi za dini, asasi za kiraia na jamii kwa ujumla katika kukabiliana na changamoto hizo." Ameongeza Mhe. Kihanga.
Kwa upande wa Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro, Enedy Mwanakatwe, amesema kuwa madhumuni ya kuadhimisha siku hii, kwanza ni kumbukumbu ya Mateso na kunyanyaswa kwa watoto wa kitongoji cha Soweto huko Afrika ya kusini wakati wa Utawala wa Kikaburu, siku ambayo watoto wa Soweto waliandamana kupinga Sheria mpya ya Makaburu katika kufundisha shule zote kwa lugha ya kigeni siku hiyo watoto waliandamana kwa nia ya kusikilizwa shida zao.
Mwanakatwe amesema baada ya mateso ya watoto hao matokeo yake askari wa Makaburu waliamriwa kuwatawanya kwa nguvu na katika kufanya hivyo walifyatua risasi na kuwauwa watoto wengi jambo ambalo ni ukatili kwa watoto.
“Tumeadhimisha haya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika lakini pia ni fursa kwetu kukaa chini na kutafakari juu ya hali ya ulinzi pamoja na ustawi wa watoto wetu kwani watoto ni nguzo imara ya jamii yoyote iliyoendelea” Amesema Mwanakatwe.
Madhimisho ya Siku ya Mtoto Afrika mwaka 2021 yanaadhimishwa kila mwaka ifikapo Juni 16 ambapo kauli mbiu ya mwaka huu imebeba ujunmbe “Mtoto ni msingi wa Taifa Endelevu; Tumtunze , Tumlinde na Kumuendeleza.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa