Waziri wa nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jaffo amewataka mameneja wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA mikoani kuacha tabia za urasimu katika utoaji wa vyeti kwa wakandarasi wa barabara za halmashauri zinazojengwa kwa sasa.
Waziri Jaffo alitoa agizo hilo Manispaa ya Morogoro wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutembelea miradi ya barabara na shule za sekondari za Kilakala na Mzumbe ya wilayani Mvomero.
Jaffo alilazimika kutoa agizo hilo mara baada ya kupata malalamiko kutoka kwa meneja wa huduma za barabara mijini (TARURA) Bw Godwin Mpinzile aliyemlaumu meneja wa TRA mkoa wa Morogoro Bi Kabuka Mwemezi kuwa amekuwa akichelewesha kuwapatia cheti cha ujenzi wa barabara kwa kumtaka kulipa kodi.
Baada ya malalamiko hayo Waziri Jaffo alimwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro Bw John Mgalula kumfuata meneja huyo na endapo ataendelea na msimamo wake atoe taarifa kwake ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.
Alisema baada ya Bunge kuondoa ongezeko la thamani VAT kwa baadhi ya vipengele bado kumekuwa na urasimu kwa baadhi ya mameneja wa TRA wa mikoa kwa kung'ang'ania na kuendelea kudai kulipwa kodi wakati ilishaondolewa.
Pia Waziri huyo aliwataka kandarasi wanaoendelea na ujenzi wa barabara za ndani za Halmashauri kuhakikisha zinakuwa kwenye kiwango chenye ubora kwani zimekuwa zikitumia fedha nyingi.
"Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara zilizoko ndani ya Halmashauri ,sitaki kuskia ndani ya mwaka mmoja barabara imeharibika ,mkandarasi atakaye haribu kazi ajue Serikali hii si ya kuchezea atachukuliwa hatua"alisema Jaffo.
Meneja wa TARURA Godwin Mpinzile alimhakikishia Waziri Jaffo kusimamia kikamilifu ujenzi wa barabara tatu za Nanenane ,Tubuyu zenye kilomita 2.4 na Maelewano yenye urefu wa mita 600 za Manispaa ya Morogoro na ujenzi huo unaghalimu kiasi cha shilingi 12.8 bilioni.
Ujenzi wa barabara hizo unafanywa kwa ushirikiano baina ya kampuni mbili ya Group Six International na kampuni ya Lukolo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa