Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo amewataka wanafunzi wa Sekondari ya Kilakala Mkoani Morogoro kuendeleza rekodi ya kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kidato cha sita na kuwataka Viongozi wa Mkoa kusimamia vema ufaulu wa mitihani ya kidato cha nne ili uweze kufanana na ufaulu wa Kidato cha sita au zaidi.
Waziri Jafo ameyasema hayo leo Mei 20 akiwa njiani kikazi kuelekea Mkoani Iringa ambapo alipita katika shule hiyo ya Kilakala na kuongea na uongozi na kisha kuongea na wanafunzi huku akiwatia moyo wanafunzi kufanya vizuri zaidi kwenye mitihani yao.
“Mimi natamani sana matokeo yenu yakitoka nikiangalia One mmefunga One hapa Kilakala , natamani sana na Mungu awabariki mmpate One ninyi nyote, zingatieni masomo na kuwaheshimu Walimu wenu”amesema Waziri Jafo huku akiwataka viongozi ngazi ya Mkoa na Wilaya kusimamia ufaulu wa Kidato cha Nne katika shule hiyo kwani haujawa mzuri sana kuanzia miaka ya karibuni.
Aidha, Waziri Jafo amesema kwa sasa Serikali ya awamu ya tano chini ya Dt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania inaendelea na ukarabati wa shule 25 kote nchini huku Mhe. Rais akiwa ametoa takribani Sh. Bil2. kwa ajili ya ukarabati huo lengo ikiwa ni kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia ili kurudisha umaarufu wa shule hizo kongwe hapa nchini ikiwemo shule ya Sekondari ya Kilakala.
Katika hatua nyingine Waziri Jafo amepokea na kuahidi kulifanyia kazi ombi la Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bi. Regina Chonjo ombi la kuufanyia ukarabati ukumbi wa Shule ya Kilakala pamoja na nyumba za walimu wanaofundisha shule hiyo ili majengo hayo yafanane na majengo mengine ya shule hiyo ambayo yamekwishafanyiwa ukarabati.
Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Mhandisi Joyce Balavuga amemuomba Mhe. Waziri Jafo Jengo, Vifaa na Wataalamu wa masuala ya TEHAMA ili Kuifanya shule ya Sekondari ya Kilakala kuwa kitovu cha Teknolojia Habari na Mawasiliano – TEHAMA kwa ajili ya kuwalea wanafunzi wa shule hiyo kisayansi zaidi Ombi mbalo limepokelewa na Waziri kuwa atalifanyia kazi.
Waziri Jafo kabla ya kuondoka shuleni hapo ametoa ofa ya chakula kwa wanafunzi wa shule hiyo kwa kuwanunulia Mchele kilo 100 na kuku 50 kwa ajili ya chakula, lengo mahususi la Ofa hiyo ni kuwatia moyo wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili kufaulu katika mitihani yao na kuleta matunda kwa Taifa la Tanzania.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa