Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amepiga marufuku Polisi jamii kukamata bodaboda zinazofanya makosa ya usalama barabarani nchini.
Waziri Lugola alipiga marufuku katika hotuba yake kwa wananchi wa Manispaa Morogoro kwenye mkutano uliofanyika hivi karibuni uwanja wa shule ya Mafisa , Manispaa ya Morogoro.
Pia Waziri Lugola amepiga marufuku Polisi wa usalama barabarani kukamata vyombo vya moto wakiwa hawajavaa sare za Jeshi.
Lugola alisema, Polisi Jamii hawana ujuzi wa kijeshi wa ukamataji wa bodaboda hivyo kuendelea kuifanya kazi hiyo ni kuwanyanyasa wananchi.
“Nimepata malalamiko mengi ninapofanya ziara zangu hapa nchini, wengi wanawalalamikia Polisi Jamii kuwaonea, kuwaomba rushwa na kuwakamata pasipofuata utaratibu unaotakiwa kijeshi, hapa Morogoro pia, katika mkutano huu wa hadhara mnayasema yale yale, sasa natangaza kuanzia leo, marufuku Polisi Jamii kukamata bodaboda” alionya Lugola.
Waziri Lugola pia alipiga marufuku baadhi ya Polisi wa Usalama barabarani ambao wana tabia ya kutovaa sare za Jeshi na kuingia barabarani au mitaani na kuyakamata magari na bodaboda.
Lugola alisema lazima polisi wafate sheria za usalama barabarani hasa wanapokamata magari yanayofanya makosa, uvaaji wa sare za Jeshi ni muhimu na unapaswa kufuatwa.
Waziri Lugola aliongeza kuwa, bodaboda au vyombo vingine vya moto, zinazovunja sheria za usalama barabarani zinapaswa kukamatwa bila kuwaonea huruma, ila ni kosa Polisi kuwanyanyasa vijana hao ambao wanapata ridhiki kupitia biashara hiyo.
Lugola alifafanua kuwa, bodaboda zinazotakiwa kuwepo kituo cha polisi ni zile zilizopo katika makundi matatu ambayo ni Bodaboda zilizohusika kwenye uhalifu, zilizotelekezwa au zilizookotwa na zilizohusika katika ajali.
Pia Lugola aliwataka waendesha bodaboda mjini Morogoro na Tanzania kwa ujumla wafate sheria za usalama barabarani zikiwemo kuvaa kofia ngumu, kutokubeba abiria zaidi ya mmoja na pia wakiendesha wanapaswa kuwasha taa.
Kwa upande wao Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo , Meya wa Maniaspaa , Pascal Kihanga pamoja Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Morogoro Mjini kichama Fikiri Juma kwa nyakati tofauti walimpongeza Rais kwa kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama kwa kuwezesha mazingira mazuri ya kufanya baishara kwa wamachinga na mama lishe .
Pia walimpongeza Rais kwa kuanzisha na kutekeleza miradi mikubwa ya kimaendeleo ikiwemo ya reli ya Mwendokasi , ununuzi wa ndege na ujenzi wa mradi wa umeme wa maporomoko ya maji ya mto Rufiji ambayo itachangia ukuaji wa uchumi na kutoa ajira kwa vijana na wananchi wengine sambamba na kumpongeza Waziri huyo kwa kufuatilia kero cha wananchi wanyonge.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa