Serikali kupitia Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Tume ya Ushindani (Fair Competition Commission) imeshauriwa kuanzisha mtaala wa somo litakalotoa elimu kwa wanafunzi juu ya kujenga jamii yenye uelewa wa madhara ya matumizi ya bidhaa bandia kutokana na ukuaji wa teknolojia duniani.
Ushauri huo umetolewa na baadhi ya walimu na wanafunzi wa shule ya Msingi Mazimbu A iliyopo katika Manispaa ya Morogoro kuwa kuanzishwa kwa mtaala wa somo hilo kutawezesha siku za usoni kujenga jamii yenye uelewa kwa kuanzia na ngazi ya chini ya familia mpaka ngazi ya juu kielimu .
Mwanafunzi wa shule ya msingi Mazimbu A anayesoma darasa la saba Irene Materni ,aliiomba Wizara hiyo kuanza mchakato wa kuanzisha mtaala wa elimu ya mlaji kwa ajili ya shule za msingi kwa lengo la kuwawezesha Wanafunzi kupata ulewa wakiwa wadogo ili wanapokuwa wakubwa waweze kukabiliana na changamoto za bidhaa bandia.
Alisema ,amejifunza mambo muhimu katika kukagua uhalisia wa bidhaa ambayo ni ufungashaji wa bidhaa, uandishi wa jina la bidhaa au nembo, usanifu wa mwisho wa bidhaa, bei ya bidhaa ambazo mara nyingi huwa na punguzo la bei, maelezo ya bidhaa ambapo mara nyingi bidhaa bandia hukosa maelezo muhimu.
Naye Mwalimu mkuu wa Shule hiyo, Anitha Nathan alisema , elimu haki na wajibu wa mlaji imetolewa kwa wanafunzi wa darasa la tano na la sita ambapo wao wataifikisha kwa wenzao wakiwa shuleni na kwa wazazi na walezi wao.
Naye Mwalimu Joha Mzuzuri alisema , walimu wa shule tano za msingi Manispaa ya Morogoro walipatiwa mafunzo ya kuwa wakufunzi wa utoaji elimu kwa klabu shuleni kuhusu haki na wajibu wa mlaji.
Mzuzuri alisema ,elimu hiyo iliendelea kutolewa kwa wanafunzi na ni hatua itakayosaidia kukabiliana na changamoto ya ununuzi na matumizi ya bidhaa zisizo na ubora zilizopo katika soko.
“ Walimu wakufunzi wa elimu hii tuliyopata nasi tumeitumia kwa kuwafundisha wanafunzi katika shule zetu ikiwemo ya Mazimbu A kuhusu elimu juu ya haki na wajibu wa mlaji” alisema Mzuzuri .
Mwalimu Mzuzuri alisema ,ili elimu hiyo iwe endelevu kwenye shule za msingi nchini ni vyema Serikali kupitia wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na wadau wengine kuanzisha mitaala wa somo hilo.
“ Tukiwajengea uwezo wa elimu wanafunzi wa shule za msingi ni rahisi elimu hii kuwafikia wazazi, walezi na jamii ambayo baadaye inakuwa yenye uelewa kwa kuanzia na ngazi ya chini ya familia mpaka ngazi ya juu kielimu “ alisema Mzuzuri.
Kwa upande wake Ofisa wa Tume ya Ushindani kutoka Idara ya kumlinda Mlaji , Emmanuel Nyanza aliwataka watanzania wawe walalamikaji wenye kuchukua hatua badala ya kunung’unika pasipo kudiriki kuchukua hatua.
Alisema ,endapo watanzania watachukua hatua ikiwa ni pamoja na kuifanyia uchunguzi bidhaa husika na kuifikisha katika vyombo vya kiuchunguzi na kisheria kama vile Tume ya Ushindani nchini (FCC) wahusika wataadhibiwa vikali.
“ Mara nyingi tunanunua vitu na bidhaa mbalimbali bila kuzifahamu au kuzichunguza vyema na hili limesababisha watu wengi kununua bidhaa zisizofaa kwao au zenye madhara kwenye afya zao” alisema Nyanza.
Hata hivyo alisema ,kwa mkoa wa Morogoro Tume hiyo imekuwa ikipokea na kuyafanyia kazi kwa haraka malalamiko ya mlaji pamoja na kuwapa elimu wafanyabiashara.
Nyanza alisema, Tume hiyo iliamua kuanzisha kwenda katika shule za msingi na kuanzisha vilabu za wanafunzi na kutoa elimu ya ulewa wa kumlinda mlaji ili visaidie pia kuelimisha jamii wanapokuwa nyumbani.
“ Tume imeamua kutoa elimu juu ya haki za mlaji kwa kuwa wanafunzi wa kikazi hiki ni kizazi cha kesho ambacho kinapaswa kuwa na ulewa juu ya madhara ya bidhaa bandia “ alisema Nyanza.
Alisema ,kwa hivi sasa Tume hiyo imetoa elimu ya kumlinda mlaji kwa kuanzia shule tano za Manispaa ya Morogoro ambazo ni Mzimbu A, Kihonda, Mzinga , Kemo na Mafiga ambapo pia imetolewa kwa shule nyingine mkoani Dodoma na na mpango mkakati ni kuifikia mikoa yote hapa nchini.
FCC imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003 na madhumuni makubwa ya uwepo wa Tume ni kukuza na kulinda ushindani wa haki katika biashara na kumlinda mtumiaji wa bidhaa na huduma dhidi ya mwenendo usiofaa katika soko.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa