MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, ambaye ni Diwani wa Kata ya Mazimbu , amegawa vitambulisho vya msamaha wa matibabu kwa wazee 83 katika kata hiyo kwa lengo la kuvitumia kwa ajili kutambulika na kupata huduma ya Afya bure katika hospitali za Serikali.
Zoezi hilo limefanyika Januari 19/2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Kata ya Mazimbu ambapo makabidhiano hayo yamefanyika kwa Wenyeviti wa Mitaa ya Kata hiyo yakishuhudiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Kata ya Mazimbu Ndugu, Isack Wella.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa Vitambulisho hivyo, Mhe. Kihanga, amewahakikishia wazee hao kuwa zoezi hili ni endelevu kwa Kata zote 29 ili kuhakikisha kila mzee aliyoko ndani ya Manispaa ya Morogoro hii anapata kitambulisho hiko.
Naye Afisa Ustawi kutoka Ofisi ya Ustawi , David Max, amewataka wazee wote waliopata vitambulisho vya msamaha wa matibabu kuanza matibabu katika ngazi ya Zahanati zilizoko katika mitaa yao hadi ngazi ya Wilaya.
Akiongea mara baada ya zoezi la ugawaji wa vitambulisho hivyo, Mwenyekiti wa Wazee Kata ya Mazimbu, Isack Wella, amewaomba Madaktari na Wauguzi kutoa huduma hiyo bila kuwanyanyasa pamoja na kuiomba Serikali kuruhusu vitambulisho hivyo kutumika kwenye huduma zote kwa maana ya kupatiwa vipimo pamoja na Dawa.
Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa Halmashauri zinazotekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungan wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kuwa wazee wote wanapata Matibabu bure kupitia Vitambulisho hivyo vya Msamaha wa Matibabu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa