Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wa Manispaa ya Morogoro, leo tarehe 05.02.2024 wametakiwa kutoa elimu ya usafi kwenye mitaa yao, sambamba na kufanya tathmini ya hali ya vyoo, na vyanzo vya maji vilivyopo kwenye maeneo hayo hivi sasa ili Manispaa iweze kuchukua hatua za kuhakikisha wananchi wake wanakuwa salama dhidi ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.
Akizungumza kwenye kikao na wahudumu hao, Afisa Afya wa Manispaa ya Morogoro, ndugu Ndimile Kilatu amewataka wahudumu wa afya kutoa elimu hiyo nyumba kwa nyumba huku wakiwasisitiza wananchi kufanya usafi kwenye miji yao na kuweka ndoo zenye koki kwa ajili ya kunawa mikono.
“Kwa wananchi wanaotumia maji ya visima, chemichemi na mito ni lazima wayachemshe kabla ya kuyatumia. Pia hakikisheni mnawapatia wananchi wenu vidonge vya kutibu maji ili waviweke kwenye maji yao ya kunywa” alisisitiza Kilatu.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Daktari Focus Maneno, amewapongeza wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha wananchi wanapata elimu za afya na kuwataka waendelee kuchapa kazi huku wakifahamu kwamba Serikali inathamini sana huduma yao na inao mpango wa kuirasimisha.
“Tujue kwamba tunalo tatizo la magonjwa ya kuharisha na macho hivyo ni lazima tupite nyumba kwa nyumba tutoe elimu ya afya ili tatizo hili liweze kuisha. Ninyi kwenye jamii mkifanya vizuri na wataalamu wa afya wakafanya vizuri kwenye Zahanati zetu na Vituo vyetu vya Afya, naamini tutatokomeza tatizo hili” alieza Daktari Maneno.
“Lakini elimu mtakayoitoa ni lazima ijikite kwenye miongozo ambayo tumewapatia ili kuepuka uwezekano wa kuzua taharuki miongoni mwa wananchi” alisisitiza Daktari Maneno.
Pia, Daktari Maneno amewataka wananchi kutoogopa kwenda kwenye vituo vya afya endapo watapatwa na ugionjwa wa kuharisha na kutapika hata kama hawatakuwa na pesa, na mara baada ya kupatiwa matibabu na kurudi kwenye makazi yao, wahudumu wa afya wawafuatilie kujua maendeleo ya afya zao.
Nao wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wamesema wao watapita nyumba kwa nyumba kutoa elimu ya usafi, watahamasisha wananchi waweke ndoo za maji zenye koki kwa ajili ya kunawa mikono na kwa wasio na uwezo wa kununua ndoo hizo watawafunza jinsi ya kutengeneza vidumu chirizi.
Aidha wameuomba uongozi wa Manispia kuhakikisha takataka zinazozalishwa mitaani na kwenye masoko zinazolewa kwa wakati ili kuepuka uchafuzi wa mazingira na magonjwa ya mlipuko pindi mvua zinaponyesha.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa