MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, ametoa kiasi cha Shilingi Milioni Moja 1,000,000/= kama ahadi aliyoiahidi kwa Taasisi ya Wildina Foundation inayojishughulisha na kuwasaidia kuwanyanyua kiuchumi pamoja na kuwaendeleza wakina Mama wanaoishi katika nyumba za Polisi Manispaa ya Morogoro inayoongozwa na Mama Yustina Mutafungwa ambaye ni mke wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro .
Hafla hiyo fupi ya kuwakabidhi fedha hizo ikiwa ni njia ya kuwaunga mkono wakina Mama wanaoishi katika Nyumba za Polisi Manispaa ya Morogoro, imefanyika leo Machi 19, 2020 Ofisini kwake.
Akizungumza na Waandishi wa habari, DC Chonjo, amesema kuwa ametoa kiasi hicho cha fedha kama ahadi yake kufuatia kuwaahidi katika mkutano walimualika wa harambee ya kuchangia fedha kwa ajili ya kupata mtaji wa kuendeleza Taasisi hiyo ikiwa na lengo la kujikwamua kiuchumi.
“Natoa fedha mimi nikiwa Mkuu wa Wilaya hii ya Morogoro,najua Taasisi hii imekuwa msaada mkubwa kwa wakina Mamam hapa mkoani Morogoro bila kusahau mimi pia Mwanamke mwenzao , fedha hizi ni ahadi yangu kwenye harambee waliyonialika , lakini natarajia kuona fedha hizi zitakwenda kutunisha mfuko wenu wa uwezeshaji wa kiuchumi wa wakina mama, natambua kwamba wakina mama ambao ni wake wa Polisi ni ndugu zetu na hawa ndio ambao wanawalinda Askari zetu wanaolinda usalama wa raia na mali zao, kwahiyo wanapokuwa na jambo lao lazima sisi Viongozi tuwaunge mkono, maana kukiwa na maugovi na mapungufu katika Familia hata hawa askari wetu wanakosa hali ya kutulinda sisi Wananchi, tunafahamu hali zetu katika mishahara ”Amesema DC Chonjo.
Aidha amesema kitendo cha kuundawa kwa Taasisi hiyo kumetokana na kujiongeza kwa Wakina Mama kwani wengi wao wanafamilia hivyo wameona ni vyema wakajiingiza katika shughuli za Ujasiriamali kwa kuuza Chakula, Mapambo , Ushonaji wa Nguo, ushonaji wa Vikapu na mikeka pamoja na kufanya shughuli nyengine ili waweze kujikomboa na kuacha utegemezi na kuzilea familia zao zikaaishi maisha bora.
Amesema kutokana na juhudi walizozionesha zilimfanya kuwaunga mkono ili waweze kufanya shughuli zao za kuongeza kipato katika Familia ukizingatia wao ni wakina Mama kama alivyo yeye na anategemea baadaye kuwaona wakiwa na maisha mazuri huku wakitembea kifua mbele.
Pi amesema kuwa hatua waliyofikia ni madhubuti ya kujenga uwezo wa wanawake waweze kujitegemea ili waweze kufanya maamuzi juu ya maisha yao na kutekeleza maamuzi hayo kwa kutumia rasilimali zilizopo bila kuingiliwa au kubughudhiwa na mtu, taasisi au chombo chochote kwa sababu tu, wao ni wanawake.
Naye Mwenyekiti wa Wildina Foundation, Bi. Yustina Wilbrod Mutafungwa, amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa upendo na moyo aliouonyesha kwa kuwakabidhi ahadi aliyoiahidi katika harambee waliyomwalika.
Amesema kuwa, mchango wake hautaenda bure, bali watautumia kwa malengo waliyokusudia ili kuweza kusongesha gurudumu mbele la kuongeza kipato katika familia za wakina mama wanaoishi katika Kambi na nyumba za Polisi.
“Tunamshukuru sana Mama yetu Chonjo, amekuwa mstari wa mbele sana kusaidia jitihada zinazofanywa na Jeshi la Polisi ukizingatia naye aliolewa na askari, hivyo kama Mwanamke na Mama mwenzetu amekuwa ni mtu wa karibu sana kwetu , kila tunapopata jambo tukimwambia amekuwa mtu wa maamuzi na kutusaidia alituahidi na leo ametekeleza lakini kwa hili la leo tutamuhakikishia kwamba tutarudi Ofisini kwake tukiwa kifua mbele kabisa kwa mafanikio tutakayoyapata kikubwa aendelee na Moyo huo huo na asituchoke pale tutakapokuwa tumekwama “Amesema Mama Mutafungwa.
Amesema lengo la kuanzisha Taasisi hiyo ni kuweza kuwanyanyua wakina Mama na wanawake wanaoishi katika Nyumba za Polisi kwani wengi wao wanaishi katika mazingira magumu na hawawezi kufanya kazi na vipato vyao ni vidogo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa