MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, amesema kasi ya ujenzi wa Stendi Mpya ya Dala Dala hairidhishi, hivyo ametoa wito kwa Mkandarasi wa mradi huo kuongeza kasi ili mradi uweze kukabidhiwa kwa Wananchi kwa muda uliopangwa.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea mradi huo leo Novemba 23, amesema bado mradi huo unashida kwani idadi ya wafanyakazi waliopo ni wachache ukilinganisha na ukubwa wa eneo na kazi zinazotakiwa kufanyika.
Aidha, amesema kuwa ifikapo tarehe 31 Desemba, 2019 pesa iliyotolewa na wafadhili kwaajili ya mradi huo itachukuliwa na wafadhili kwakuwa mda wa mradi utakuwa umeisha hivyo kuna haja ya kuhakikisha kazi inafanyika usiku na mchana ili pesa hiyo isiondoke na mradi ukamilike kwa wakati.
"Mkandarasi kwakweli sijaridhishwa na kasi ya ujenzi, pia huwezi kuwa na mradi mkubwa kama huu harafu ukawa na wafanyakazi wachache unafikiri kweli kwa muda tulio nao tutaweza kukamilisha kwa wakati? niwaombe ongezeni vibarua muda umekwisha hii asilimia 40% ya ujenzi wa Stendi mliyoniambia sijaridhika nayo, nataka nikija nikute kazi zimefanyika kwa kiwango kikubwa, tambueni pesa za mradi huu zina masharti mwezi Desemba ujenzi uwe umekamilika ili wananchi waweze kupata huduma,haiwezekani Mhe. Rais Dkt John Magufuli aje kufungua mradi akutane na mabango"Amesema DC Chonjo.
Amemtaka Mkandarasi, mshauri wa mradi pamoja na Mhandisi wa Manispaa kukaa pamoja katika vikao vyao ili kuweza kuangalia vipaumbele vya ujenzi, kwani kitu cha kwanza kilichotakiwa kujengwa ni Stendi na sio jengo la utawala.
Amesema kitu muhimu kilichohitajika katika ujenzi wa Jengo la utawala ilikuwa ni Choo, miundombinu ya maji pamoja na umeme lakini sio jengo la utawala ambalo litakuwa na watu wachache kuliko Stendi ya Daladala.
Aidha DC Chonjo amesema Bilioni 5.2, mkandarasi alizochukua kwaajili ya ujenzi wa stendi hiyo, mradi huo ulipaswa uwe na huduma zote kama zilizopo kwenye Stendi ya zamani kwani haitakuwa jambo rahisi kuwaambia Wananchi wahamie Stendi mpya harafu huduma muhimu zinakosekana itakuwa ni jambo baya na litaleta mtafaruku kwa Wananchi.
Amesema anataka kuona Stendi hiyo ikiwa na maeneo ya Vioski , maeneo ya Wajasiriamali wadogo wadogo wamamchinga, wauza urembo pamoja na Mama lishe na Baba lishe, hivyo kama vitu hivyo vitakosekana itakuwa haina maana ya kuwepo na mradi mkubwa kama huo.
DC Chonjo amewaagiza Wahandisi wa TARURA, Mshauri wa mradi pamoja na mhandisi wa Manispaa kukaa kwa pamoja waone ni namna gani mradi huo utakavyo pokelewa kwa Wananchi.
Kwa upande wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesema kasi ya ujenzi ipo chini hivyo amemtaka mkandarasi kuongeza vibarua kama Mkuu wa Wilaya alivyoshauri ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Amesema ingependeza zaidi kama wangeanza na ujenzi wa vibanda vya maduka vya wafanya biashara kuliko kuendelea kuweka nguvu katika ujenzi wa jengo la Utawala ambalo sio kipaumbele katika mradi huo.
"Hapa mshakosea lakini niwaombe bado muda mnao hakikisheni mnaweka nguvu katika ujenzi wa Stendi ili hawa wananchi waweze kutumia kwani jengo la utawala lilikuwa halina umuhimu kwa sasa zaidi ya Stendi, ongezeni kasi tunachotaka sisi ni kuona matokeo ili hii pesa tuliyopewa kwa masharti tunufaike nayo kabla haijachukuliwa, ikichukuliwa mradi tunaukosa na nyie pia hamtapata pesa" Amesema Mhe. Kihanga.
Naye Mshauri wa Mradi , Mhandisi. Antonio Mkinga, amesema mradi huo ulitakiwa kumalizika Mei 25, 2020 lakini kati kati ya Mwezi Oktoba, 2019 kulitolewa agizo la kutaka mradi ukamilike ifikapo Desemba 31, 2019.
Amesema walishamwandikia barua mkandarasi wa mradi ya kumuelekeza kuongeza vibarua lakini cha kushangaza hadi sasa bado vibarua hao hawajaongezwa.
Aidha , amemtaka Mkandarasi wa mradi kuongeza mashine pamoja na vifaa kwenye eneo la mradi ili kasi ya ujenzi iende na kukamilisha mradi kwa wakati na kuweza kutoa huduma kwa wananchi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa