MKUU wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo amewaagiza watendaji wa mitaa na kata katika Manispaa ya Morogoro kushirikiana na madiwani kuhakikisha miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inakuwa salama dhidi ya hujuma mbalimbali katika maeneo yao.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa agizo hilo katika kikao cha pamoja kati ya madiwani , watendaji wa kata, viongozi wa halmashauri ya Manispaa na wa Tanesco mkoa wa Morogoro katika kikao kilichofanyika kwa ajili ya kujadili namna ya kudhibiti hujuma za miundombinu ya shirika hilo.
Alisema , Shirika la Tanesco mkoa wa Morogoro limekuwa likikabiliwa na changamoto ya kuhujumiwa kwa miundombinu yake zinazofanywa na watu wasiojulikana na kurudisha nyuma jitihada za shirika hilo za kuwaletea maendeleo wananchi.
Katika kusaka suhuhu hiyo aliutaka uongozi wa Tanesco mkoa kusaidia kupata orodha ya watumishi waliokuwa wameondolewa kwenye ajira ikiwa ni kwa kustaafu, watumishi hewa , vyeti vya kugushi na wengineo na orodha hiyo iwasilishwe Kituo kikuu cha Polisi kwa ajli ya ufuatiliaji wa karibu juu ya nyendo zao.
Hata hivyo alisema, ili kukabiliana na hujuma hizo, Serikali ya wilaya ya Morogoro imeamua kupiga mafurufu shughuli za kibinadamu kando kando na miundombinu ya Tanesco , kuzuia misumeno ya moto ikiwa ni pamoja na Tanesco kuongeza suala la utoaji wa elimu kwa wananchi .
Kwa upande wake , Meneja wa Tanesco mkoa wa Morogoro Mhandisi Hassan Said katika taarifa yake katika kikao hicho alisema , katika kipindi cha miaka miwili na nusu zaidi matukio 22 ya kuhujumiwa kwa miundombinu ya Tanesco yamejitokea ikiwemo ukataji wa nguzo za umeme, wizi wa nyaya, na uharibifu wa transfoma.
“ Mwaka 2016 pekee kulikuwa na matukio nane ya kuhujumiwa kwa miundombinu ya Tanesco ndani ya Manispaa ya Morogoro ,mwaka 2017 matukio manne na kwa mwaka huu hadi kufikia mwezi Mei ni matukio sita jambo hili hata mwaka haujamalizika , na kibaya zaidi licha ya juhudi za kushirikiana na vyombo vya dola hakuna mtu aliyekamatwa " alisema Mhandisi Said.
Nao baadhi ya wajumbe wa kikao hicho ambao wengi wao walikuwa ni madiwani kwa nyakati tofauti walitoa ushauri kwa Tanesco kwa kuitaka kuboresha mahusiano na jamii, kuzifanyia kazi haraka kero za wateja wao ikiwa na kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa wanapokuwa katika majukumu yao ya kazi .
Diwani wa Kata ya Boma , Amir Nondo alisema , ni vyema wafanyakazi wa Tanesco wanapokuwa na majukumu yao mitaani wapitie ofisi za mitaa kutoa taarifa ili wananchi watambue uwepo wao kwani bila kufanya hivyo waaarifu nao wanatumia mwanya huo kujipenyeza kuharibu miundombinu ya shirika .
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa