MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, amewataka Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Manispaa ya Morogoro, kuchapa kazi kwa kufuata katiba ya Nchi na Miongozo ya kiutendaji ya Serikali za Mitaa na maadili ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Watendaji wa Serikali katika maeneo yao ya kazi ili kuwaletea Wananchi maendeleo na kutatua kero zao kwa wakati.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Januari 7, 2020, katika Semina elekezi ya mafunzo kwa Wenyeviti wa Mitaa, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa , amesema kuwa ili maendeleo yaje kwa haraka lazima wenyeviti na watendaji wawe kitu kimoja na kuzingatia misingi ya Uongozi ya Utawala bora.
Amesema Wenyeviti wa Mitaa hawana tofauti na Viongozi wowote wanaosimamiwa na Serikali katika ngazi za Wilaya, Mkoa na Taifa, hivyo kila mmoja wao afuate misingi ya Uongozi katika kutoa huduma kwa Wananchi.
"Nisingependa kusikia Mwenyekiti wa Mtaa anauza Ardhi za Wananchi, anadhulumu mashamba ya wananchi, mimi ni msimamizi mkuu wa Serikali katika Wilaya sitalifumbia macho suala hilo, ifahamike kuwa kumekuwepo na tabia ya wenyeviti wa Mitaa wasio waadilifu katika pesa pale wananchi wanapofika kwao kuhitaji huduma fulani, wenyeviti mnapaswa kuwa wazalendo na kuishi kwa kuwa waadilifu na wachapa kazi kwa wananchi waliowachagua" Amesema DC Chonjo.
Amewataka Wenyeviti wa Mitaa na Wajumbe wao kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo katika kuwatumikia wananchi ili kuendana na kasi ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Hata hivyo alichukua nafasi ya kuwapongeza wenyeviti hao kwa kuchaguliwa na kuwaeleza kuwa ushindi wao haikuwa kazi rahisi hivyo amewataka wafanye kazi kwa bidii ili wasikiangushe chama kilichowaweka madarakani.
Amesema imani yake ni kwamba baada ya mafunzo hayo wenyeviti wa mitaa watakuwa tayari kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria, kanuni, Taratibu na miongozo mbalimbali inayotolewa na Mamlaka na kupunguza migogoro pamoja na malalamiko yanayojitokeza yanayopelekea wananchi kuyafikisha kwa Mkurugenzi, Mkuu wa Wilaya au Mkoani.
" Naimani pia mtaboresha mahusiano mazuri na watendaji wenu wa Mitaa na Kata na mtaenda kutekeleza shughuli zenu kwa ushirikiano wa karibu , hakikisheni mnazingatia misingi ya Utawala bora katika utendaji wenu wa kazi bila upendeleo wa aina yoyote wa kisiasa, kidini na kikabila na mumtangulize Mwenyezi Mungu kwa kila jambo" Ameongeza DC Chonjo.
"Wenyeviti wa Mitaa nyie ni wawakilishi katika Jamii na hamna budi kuwashirikisha wale mnaowaongoza ili kwa pamoja kupiga hatua ya kushinda maadui wa Taifa yaani Umasikini, Ujinga , Maradhi na pia rushwa ambayo sasa ndiye adui wa haki na anachangia katika kudhoofisha vita dhidi ya wale maadui wetu wale watatu wa awali" Ameongeza DC Chonjo.
Pia Mkuu wa Wilaya huyo, amesema hali ya usafi katika Mitaa bado hairidhishi, amewataka wenyeviti wasimamie kikamilifu vikundi vya uzoaji taka na kufuata sheria ya usafi ili kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na wale watakao kiuka sheria wafikishwe kwake na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amemshukuru na kumpongeza DC Chonjo kwa kufungua mafunzo hayo, huku akisema ili kutekeleza dhana ya Uongozi unaolenga kumletea mwananchi maendeleo endelevu, wenyeviti wa mitaa wanapaswa kuzingatia maadili ya uongozi na pia misingi ya Utawala bora ikiwamo kutenda haki kwa kuzingatia Utawala wa Sheria na kutimiza wajibu wao kikamilifu.
" Naimani mafunzo haya yatawasaidia kuboresha mahusiano mazuri na watendaji wenu wa Mitaa na Kata na mtaenda kutekeleza shughuli zenu kwa ushirikiano wa karibu , hakikisheni manazingatia misingi ya Utawala bora katika utendaji wenu wa kazi bila upendeleo wa aina yoyote wa kisiasa, kidini na kikabila na mumtangulize Mwenyezi Mungu kwa kila jambo" Ameongeza Sheilla .
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesema kama wenyeviti hawatakuwa na maadili basi hata maendeleo kwenye mitaa yao watayasikia kwenye bomba hivyo amewataka wenyeviti kuhakikisha wanatunza na kusimamia vyema miradi iliyo katika maeneo yao ili iweze kuwanufaisha wananchi na kuleta maendeleo katika mitaa yao.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro, Fikiri Juma, amewataka wenyeviti wa Mitaa wasiwe kero kwa wananchi badala yake wawe mfano bora wa kuhakikisha maendeleo kwa wananchi yanapatikana kwa haraka.
"Nyie ni wenyeviti mmepewa mamlaka makubwa katika mitaa yenu , tumieni ushawishi na mamlaka mliyonayo kuhakikisha mnawatunzia siri za faragha wale mnaowaongoza, hiyo ndiyo sifa ya kiongozi, mtaa mchafu wewe upo, maji hakuna wewe upo matukio ya ukatili yanatokea wewe upo, badilikeni msifanye kazi kwa mazoea tunataka matokeo chanya wananchi waliwaamini wakawapatia ridhaa itumieni hiyo nafasi vizuri tumsadie Mhe. Rais katika kuwaletea maendeleo wananchi" amesema Fikiri
Afisa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Fredrick salwa, amewataka wenyeviti kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizopo huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano na TAKUKURU .
"Mihuri mliyopewa siyo ya kujinufaisha, toeni taarifa ya vitendo vya rushwa , mwananchi anatarajia kuona ukipambana na vitendo vya rushwa, morogoro bila vitendo vya rushwa inawezekana' Amesema Fredrick.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa