Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Regina Chonjo amewataka wananchi wa Manispaa kutumia muda uliobaki kujiandikisha katika daftari la uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili waweze kutumia haki yao kuchagua viongozi.
Dc Chonjo ameyasema hayo wakati alipotembelea vituo vya uandikishaji vya kata ya Kihonda mtaa wa Kilombero,Kata ya Kilakala mtaa wa Bigwa Sokoni,kisiwani,kilakala,Kata ya Mazimbu mtaa wa Darajani , Nguzo na kuwataka wananchi kutumia haki yao ya Kidemokrasia ya kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo.
“Hivyo ni muhimu kwa kila mwananchi kushiriki kwakuwa inaamua hatima yake ya kujiletea maendeleo ambayo Mhe. Rais John Magufuli amekuwa akipambana kwaajili ya watanzania,” alisema Dc Chonjo.
Akitoa taarifa ya mwenendo wa zoezi la uandikishaji Msimamizi wa Uchaguzi Manispaa ya Morogoro,Waziri Kombo ameeleza kuwa zoezi la uandikishaji linaendelea vizuri na hadi sasa wananchi 108,594 sawa na asilimia 61.2 wameshaandikishwa katika vituo mbalimbali na wameweka mikakati mbalimbali kuhakikisha wanafikia lengo la uandikishaji wananchi 177,000.
Chonjo amewahimiza wananchi aliowakuta katika vituo alivyotembelea kuwahimiza vijana wao ambao umri wao ni zaidi ya miaka 18 kuhakikisha nao wanajiandikisha ili waweze kupata nafasi ya kuchagua viongozi ambao watawaletea maendeleo.
Aidha DC Chonjo pamoja na kutembelea alizungumza na wananchi kujua changamoto zao katika uandikishaji huo na pia kuwahamasisha kuwashauri na watu wengine kujitokeza.
Manispaa ya Morogoro ilianza zoezi la uandikishaji tarehe 8/10/2019 na zoezi hilo litahitimishwa ifikapo tarehe 14/10/2019.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa