Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro , Sheilla Lukuba wametembelea kituo cha watoto yatima cha Mgolole na kambi ya wazee ya Fungafunga na kutoa mahitaji ya watoto na TV aina ya Samsung katika kituo cha wazee.
Akikabidhi vitu hivyo vyenye thamani ya Tsh 1,008,000.00 katika kituo cha watoto yatima Mgolole Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, amesema kuwa Ofisi yake na Manispaa kwa ujumla iko pamoja nao na itaendelea kushirikiana nao kwa mazuri na changamoto yeyote itakayojitokeza katika makazi ya watoto hao, hivyo wasisite kutoa taarifa pale wanapokuwa na tatizo lolote.
“Nimefurahishwa sana na huduma mnazowapatia watoto wetu, kwakweli mnastahili pongezi kubwa, ni wachache wenye moyo kama wenu wa kuwasaidia hawa watoto, msikate tamaa endeleeni na malezi bora mwenyezi mungu atawabariki sana chukueni hiki kidogo tulichowaletea ikiwa ni sehemu yetu ya kusherekea mwaka mpya na watoto wetu wajisikie huru na amani badala ya kuwa wapweke”Amesema DC Chonjo.
Pia amempongeza mlezi wa kituo hicho, Sister Palagia Maria, kwa kuwa na malezi mazuri kwa watoto hao wanaoletwa kwenye makazi hayo kutoka katika mazingira hatarishi.
Aidha Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema kuwa huo ni mwendelezo wa ahadi zilizotolewa na Mkuu wa Wilaya kwa kushirikiana vyema na Uongozi wa Manispaa ya Morogoro huku akisema kuwa tayari baadhi ya ahadi zimekwisha tekelezwa na zawadi nyingine kutoka kwa wahisani hivyo amemtaka mlezi wa makazi hayo kuendelea na moyo wa kuwasaidia watoto hao hadi pale watakapo pata mwanga wa maisha yao.
“Watoto niwaombe msome sana mkizingatia hakuna urithi zaidi ya elimu, Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Rais Dkt. John Magufuli imeweka mpango wa elimu bila malipo msome sana ili nanyi baadae muweze kuwa na maisha mazuri na kuendesha familia zenu” Amesema Sheilla.
Naye, Mlezi wa makazi hayo, Sister Palagia Maria, amemshukuru Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi ikiwamo Ustawi wa Jamii kwa kuwa karibu nao huku akiwataka wasikate tamaa kwani wao wanategemea pia misaada kutoka kwa wahisani.
Mbali na kutoa chakula pamoja na Vinywaji katika Makazi ya Mgolole, Mkurugenzi Sheilla amepata nafasi ya kutembele kituo cha kulelea Wazee wasiojiweza cha Funga Funga kilichopo Manispaa ya Morogoro na kutoa zawadi ya TV Flat Screen na king’amuzi cha Star Times vyenye thamani ya Tsh 670,000.00.
Amesema lengo la kutoa Tv hiyo ni kuwafanya Wazee hao waweze kuangalia taarifa mbali mbali za miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya tano chini ya Mhe. Rais Dkt. John Magufuli.
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi Kituo cha Funga Funga, Bi Yolanda Komba,amemshukuru Mkurugenzi na Idara ya Ustawi wa Jamii kwa kuwa karibu na kuwasaidia katika huduma mbali mbali ikiwamo kuwapatia msaada na kuwajali wazee hao wenye mahitaji muhimu hivyo anamtakia kazi njema katika kutekeleza majukumu yake na kuanza mwaka mpya kwa mafanikio zaidi.
Naye Mwenyekiti wa Wazee hao, Mzee Joseph Kaniki, ameushukuru Uongozi wa Manispaa ya Morogoro kwa kutekeleza kile walichokiomba huku akizidi kumuombea Mhe. Rais Magufuli afya njema ili aweze kuiongoza vyema Tanzania katika kufikia maendeleo hususani uchumi wa Kati na wa Viwanda.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa