MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kuboresha huduma za afya katika Kituo cha afya cha Uhuru (Nunge), kufuatia kituo hicho kuzidiwa na Wagonjwa.
Kauli hiyo ameitoa Novemba 12 wakati wa ziara ya kukagua na kuzungumza na Uongozi wa Kituo cha afya cha Uhuru (Nunge) kufuatia kituo hicho kuzidiwa na Wagonjwa na ufinyu wa eneo.
“Tumejionea hali ilivyo, tumegundua wagonjwa wanaofika hapa wanafikia 280 hadi 300 sasa idadi hii ni kubwa sana, kwahiyo tumekubaliana na Manispaa tujenge Ghorofa pamoja na kuongeza idadi ya madaktari , watumishi na wauguzi, lakini pia tumefikiria kuwe na utaratibu katika vituo vyetu vya afya wawe wanabadilishana wataalamu wanapoona kuna sehemu inapwaya ili kuwe na huduma ambayo haitasubiria maelekezo kutoka ngazi za juu, hili litasaidia sana kutoa huduma bora kwa wagonjwa wetu” Amesema DC Msulwa.
Katika hatua nyengine, amesema watawasiliana na Wizara ya afya kupitia Bohari ya dawa waongeze dawa za kutosha ili kuweza kumudu huduma zinazotolewa.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, ameahidi kukarabati Kituo cha Afya cha Uhuru (Nunge) kuwa ghorofa ili kupunguza adha ya Wagonjwa katika Kituo hicho.
Lukuba, amesema katika kipindi hiki ambacho anatafakari jinsi ya kufanya ukarabati huo , ameandaa eneo la Karibu na Mango Garden ambalo litatumika kwa ajili ya kutolea huduma ya mama na mtoto.
“Mkuu wa Wilaya ametoa ushauri, tumeupokea , na tunaangalia eneo la wazi ambapo tunatarajia kutenga eneo la Mango Garden kwa ajili ya kuhamisha huduma za Mama na Mtoto kuhamia huko ili kupisha huduma nyengine ziendelee, lakini tutakarabati hapa kwa kujenga Ghorofa ili tuzidi kuimarisha huduma za afya kutokana na idadi kubwa ya Wagonjwa wanaokuja hapa kupata huduma” Amesema Lukuba.
Aidha, amewataka Madaktari na wauguzi wafanye kazi kwa bidii ikiwamo kutumia lugha nzuri kwa wateja wao kwani wagonjwa wanapokwenda kupata huduma wanahitaji lugha nzuri ili waweze kupata faraja.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa