Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, amezindua stendi ya daladala Kaloleni na kuwataka wananchi kutunza miundombinu iliyopo kwa sababu ujenzi unatokana na kodi.
Kauli hiyo ameitoa leo Novemba 06/2020, wakati wa uzinduzi wa Stendi ya Daladala ya Kaloleni iliyopo Kata ya Mji Mpya Manispaa ya Morogoro.
Msulwa, amesema kuwa licha ya kuwa haki yao, njia moja wapo ya kuthamini fedha zao ni kulinda miundombinu iliyopo na inayoendelea kujengwa.
“Tatizo kubwa tulilo nalo ni kushindwa kutambua haki na wajibu wetu kama walaji, hiyo ndiyo sababu inayotufanya kugharamia vitu ambavyo kama tungevitunza vizuri tusingetarajia kupata gharama hizo, kwahiyo ni wajibu wetu kuthamini fedha zetu maana zinatokana na kodi zetu wenyewe" Ameongeza kusema DC Msulwa.
“Manispaa ya Morogoro ni Mji Kongwe sana , kwa hili lililofanyika leo naupongeza sana Uongozi wa Manispaa ya Morogoro kwa kuonesha na kuufanya Mji huu kuwa sura ya Manispaa, lakini niseme unapokuwa na Uongozi mzuri ngazi ya Kitaifa, Jimbo na Kata unatengeneza uelekeo mzuri wa kutengeneza maendeleo kwa wananchi au taasisi husika, kwahiyo uchaguzi umekwisha, matokeo tumeyasikia na Viongozi wetu wameshaanza kufanya kazi lakini tunasubiria waapishwe ili waweze kujipanga vizuri ” Amesema Msulwa.
Aidha, amesema lengo la Manispaa hii ni kuwa Jiji hivyo ni lazima miundombinu iweze kuboreshwa licha ya kuwa zipo changamoto zitakazojitokeza.
“Hatuwezi kukaa katika Manispaa kwa miaka 32 na tukaendelea kukaa kwa muda mrefu kabla ya hatujafika kiwango cha kuwa Jiji, lakini ukishakuwa Jiji lazima utarajie changamoto mbalimbali, changamoto hizo pia zinaweza kugeuka kuwa fursa , kwahiyo hatua ambazo Manispaa imezichukua zinatufanya kuelekea kuwa Jiji, nafahamu ukiachia stendi hii ya Kaloleni, kuna Stendi kuu ya Daladala Mafiga, Soko Kuu la Kisasa, na miradi mingine ambayo inaendelea nawapongeza sana Manispaa, Wahandisi wa miradi kwa kazi kubwa na nzuri mnazo fanya,””Ameongeza DC Msulwa.
Pamoja na hayo amesema ni vizuri pia Mkurugenzi wa Morogoro Vijijini kufika hapa na timu yake ya Uongozi ili nao waweze kujifunza na wao wakajenge Stendi kama hii kwa ajili ya kurahisisha huduma za usafiri kwa Wananchi wao.
Mwisho , DC Msulwa, ameahidi kiasi cha Shilingi Milioni Moja kwa ajili ya ukarabati wa Kituo kidogo cha Polisi cha Mji Mpya.
Naye Kaimu mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Michael Waluse, mbali na kushukuru kwa pongezi zilizotolewa katika ofisi yake, ameahidi kushirikiana na Uongozi wa Daladala wa Stendi hiyo kwa yale yote yatakayojitokeza kuhusiana na Stendi hiyo.
Waluse, amesema kuhusu Ukarabati wa Kituo kidogo cha Polisi kilichopo jirani na Stendi hiyo, katika vikao swala hilo litajadiliwa na kuona ni jinsi gani Manispaa itakavyoweza kushiriki katika hatua hiyo ya ukarabati ili iendane na hadhi ya Stendi hiyo kwani Jeshi la Polisi ndio watu wa kwanza katika kulinda amani katika eneo hilo.
Kwa upande wa Msimamizi wa fedha za mkopo wa Benki ya Dunia chini ya fedha za uboreshaji Miji ( Urban Local Government Strengthening Program (ULGSP) na Mhandisi wa TARURA Manispaa ya Morogoro, James Mnene, amesema mradi huo umegharimu kiasi cha Shilingi milioni 644 ambapo ujenzi wake ulianza Aprili 28/2020.
Mnene, amesema mkandarasi Nandhra amekamilisha Ujenzi huo kwa asilimia mia moja kama ilivyoonekana wakati wa ukaguzi kabla ya kuzinduliwa.
“Mradi umekamilika kwa asilimia mia moja kama mnavyoona,lakini kazi ambayo imebakia ni kuweka alama za kuongoza magari lakini kazi hizi zote zitafanyika katika kipindi cha matazamio,mpaka sasa Mkandarasi ameshalipwa shilingi milioni 566 sawa na asilimia 74.9 na kiasi kilichobakia atalipwa baada ya kuwasilisha madai yake ya mwishoni na matumaini ya Manispaa ya Morogoro katika Stendi hii ya Daladala ni kutoa huduma bora ya usafiri kwa magari ya Daladala yapatao 50 na kuongeza Manispaa mapato na hadi sasa hakuna kipingamizi chcochote cha kutofanya stendi hii kutotumika “ Amesema Mnene.
Hata hivyo, Diwani mteule wa Kata ya Mji Mpya, Emmy Kiula, amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Bakari Msulwa , kwa kukubali ombi lake la kukarabati Kituo kidogo cha Polisi cha Kata ya Mji Mpya kufuatia Mkuu wa Wilaya kuahidi kiasi cha Shilingi Milioni moja.
Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Daladala Mkoa wa Morogoro, Hemed Ntengwa, amesema Stendi hiyo ilikuwa changamoto sana lakini kwa sasa watafanya kazi vizuri na kuitunza miundombinu ya Stendi hiyo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa