Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, mheshimiwa Rebbeca Nsemwa, tarehe 15.02.2024 ametembelea eneo la ujenzi wa machinjio ya muda ya Manispaa ya Morogoro na kumtaka Mkurugenzi wa Manispaa kuhakikisha mradi huo unakamilika mapema ili wananchi waanze kunufaika nao.
Akiwa katika eneo hilo lenye ukubwa wa hekari 83 lililotengwa na Manispaa mheshimiwa Nsema alipokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa, kuhusu shughuli zinazofanyika, na ambazo zinatarajiwa kuendelea kufakwa mahali hapo.
Mkurugenzi wa Manispaa, ndugu Ally Machela alisema katika eneo hilo patajengwa machinjio ya kisasa, mradi ambao kwa sasa andiko lake limeshawasilishwa kwenye Wizara husika kwa ajili ya kushughulikiwa.
“Kabla mradi wa machinjio ya kisasa haujaja kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo, na Uvuvi, sisi kama Manispaa mwaka huu tumeleta hapa shilingi milioni 150 kwa ajili ya kujenga machinjio ya muda, eneo la mnada, na mazizi ya kufugia wanyama, na katika bajeti yetu ya mwaka 2024/2025 tumetenge shilingi milioni 350 kwa ajili ya kufungua barabara inayokuja kwenye eneo hili. Ni imani yetu kwamba tukifanya haya tutawavutia hata Wizara ya Mifugo kutuletea machinjio ya kisasa mahali hapa” alifafanua Machela.
Katika hatua nyingine, ndugu Machela amesema TANESCO ndani ya wiki ijayo watafikisha Transfoma ya umeme eneo hilo na umeme utaanza kuwaka.
Vilevile, amesema wataalamu wa bonde la mto Ruvu walifanya utafiti na kubaini maeneo matatu ambapo panaweza kujengwa visima vitatu, na Manispaa tayari imeshapata mfadhili ambaye atasaidiana na Ofisi yake kujenga visima hivyo.
Maeneo mengine ambayo Mkuu wa Wilaya ameyatembelea ni pamoja na jengo la wodi ya wazazi kwenye Zahanati ya Kihonda, na jengo la utawala la shule ya Sekondari Uluguru, miradi ambayo ilitekelezwa kwa nguvu za wananchi na Ofisi ya Mkurugenzi inatarajia kuikamilisha.
Akiwa kwenye miradi jengo la utawala la shule ya Uluguru, mheshimiwa Nsemwa amepongeza juhudi za Mheshimiwa Diwani kwa kuhamasisha wananchi wake kuchangia shughuli za maendeleo, na walimu kwa kutunza mazingira ya shule hiyo.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa