DIWANI wa Kata ya Mkundi, Mh. Seif Chomoka, amesema ili bidhaa ziweze kuuzika ni lazima wajasiriamali wajikite katika kujitangaza na kutafuta masoko.
Kauli hiyo ameitoa Machi 04/2023 akizungumza na Vikundi vya Wajasiriamali vilivyojitokeza katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Kata ya Mkundi.
Akizungumza juu ya kuwakomboa wajasiriamali wa Kata hiyo, Mhe. Chomoka amesema ataandaa maonesho ya vikundi vyote vya wajasiriamali kwa kushirikiana na Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi Kata pamoja na Uongozi wa Ofisi ya Kata na Uongozi wa Jukwaa ili kuweza kutoa fursa kwa wajasiriamali kujitangaza.
Amesema katika kufanikisha hilo, ataomba ushirikiano kwa viongozi mbalimbali wa Manispaa kuhudhuria katika maonesho hayo ikiwemo na wadau wengine kwa ajili ya kuwatambulisha wajasiriamali wake na kuweza kupata masoko.
" Maonesho haya kwa mara ya kwanza nitagharamia mimi kwa fedha zangu kila kitu, lengo kujitangaza, shauku yangu ni kuona wanawake wa Mkundi wananyanyuka kwa nguvu, nataka kufanya kazi na wanawake wa Mkundi, nitahakikisha kuwa malengo yangu yanafanikiwa kwani nilishatoa mkopo wa milioni 5 ili vikundi vikopeshane , huu ndio mkakati wangu " Amesema Mhe. Chomoka.
Aidha Chomoka, amesema kuwa maonesho hayo yatakuwa yakifanyika kila baada ya miezi 3 na imani yake baada ya kufanyika na kufanikiwa basi wajasiriamali wataweza kugharamia kiasi cha fedha kidogo kuendesha maonesho hayo kwa vipindi vijavyo.
Katika hatua nyengine, ametoa fursa kwa wajasiriamali wa sabuni kuwa kwa sasa masoko yao yatakuwa katika Taasisi zake anazoziendesha ikiwemo Chuo cha St. Joseph, MSJ pamoja na Shule ya A-Plas.
"Nimetangaza fursa kwa wajasiriamali wanaotengeneza sabuni, kuanzia leo, nataka nikutane nao Ofisi kwangu tukubaliane kufanya biashara kupitia Taasisi zangu ninazoendesha, hawa ninawapa masoko moja kwa moja nataka wanawake wa mkundi wajikomboe na hii ndio dhana ya Uongozi ya kuwatumikia na kuwanufaisha wale unaowaongoza" Ameongeza Mhe. Chomoka.
Naye Katibu wa Jukwaa la Wanawake Manispaa ya Morogoro, Clara Kapungu, amewataka Viongozi wa Jukwaaa kutumia fursa zilizopo katika kuvikwamua kiuchumi vikundi vyao.
Kwa upande wa Katibu aliyemaliza muda wake , Paulina Mbawala, amempongeza Mhe. Diwani kwa kuwajali wanawake wa Kata ya Mkundi huku akimuahidi kutoa ushirikiano mkubwa katika kutimiza ndoto zake za kuwasadia wanawake wa Kata hiyo.
Katika maadhimisho hayo, Vikundi vya wajasiriamali vilipata nafasi yha kuonesha bidhaa zao ambazo wamekuwa wakizizalisha.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa