Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Selemani Jaffo ameonyesha kufurahishwa na ujenzi wa soko kuu la kisasa katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro katika ujenzi ambao umekamilika kwa asilimia 99 ambapo umegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 17.6
Akizungumza mara baada ya kutembelea na kuona maeneo mbalimbali katika soko hilo Mhe. Jaffo amesema kuwa licha ya kuwepo na ujenzi wa miradi ya masoko katika Mikoa ya Mtwara, Dodoma, Njombe na Dar es Salaam ujenzi wa soko la Kisasa Manispaa ya Morogoro ni wa kipekee na wenye viwango vya hali ya juu kutokana na ujenzi huo kuwa umezingatia mahitaji ya wafanyabiasha wanataka nini katika soko hilo.
“Mimi huwa nakuja kukagua kazi sio kutembelea na nimefika mara nyingi katika soko hili,awali nilikuwa siridhishwi na kasi ya ujenzi ila leo binafsi nimefurahishwa sana baada ya kufika hapa na kuona jinsi wakandarasi wetu wazawa walivyoweza kujenga kwa ubora unaoridhisha. Hiki ni kitega uchumi kikubwa sana kwa Halmashauri na kitabadili mandhari ya Manispaa hii,kwa aliyefika hapa miaka mitano iliyopita leo hii akija anaweza kupotea hii ni heshima kubwa sana aliyotupatia Mhe.Rais Dkt John P.Magufuli kwa kuamua kutupa fedha za mradi mkubwa kama huu.”Alisema Jaffo.
"Nampongeza sana Mhandisi aliyesimamia ujenzi huu,pia nawapongeza viongozi na watumishi wote wa Manispaa ya Morogoro kwa ushirikiano mliouonyesha katika utekelezaji wa mradi huu ,hii inaonyesha jinsi gani mlivyo makini katika usimamizi wa miradi,Manispaa ya leo siyo jana angalia sasa mna stendi ya Msamvu,mmejenga stendi ya daladala,haya ni mafanikio makubwa sana katika Serikali ya awamu ya tano"Aliongeza Mhe.Jaffo.
Aidha Mhe. Jafo ameahidi kushughulikia changamoto ya msamaha wa ongezeko la thamani VAT na kuhahidi kuifikisha katika mamlaka husika kwa kuwa miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia haitakiwi kutozwa kodi.
“Lengo la miradi hii ni kwa ajili ya kukuza Miji na kuzijengea Halmashauri uwezo wa kujitegemea swala la msamaha wa VAT ni changamoto inayoikabili miradi mingi inayosimamiwa na TAMISEMI na hapa naona tena changamoto hii inajirudia licha ya Mheshimiwa Rais kutoa maelekezo kuhusiana na suala hili. Naomba nichukue changamoto hii na nitaiwasilisha kwa Waziri wa Fedha kwa utekelezaji."Alieleza Mhe.Jaffo.
Mradi wa soko kuu unatarajiwa kuingizia Halmashauri mapato ya zaidi ya shilingi Bilioni 2.3 kwa mwaka na hii itapunguza kutegemea ruzuku kutoka Serikali kuu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa