Kamati ya fedha ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita akiwemo Mbunge wa jimbo la Geita Joseph Kasheku maarufu kama msukuma na mkuu wa Wilaya ya Geita Josephat Maganga wameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kubuni na kusimamia miradi mikubwa ya kimkakati ambayo itasaidia kuongeza mapato ya Halmashauri hiyo.
Pongezi hizo walizitoa baada ya kamati hiyo kufanya ziara ya kimafunzo ambapo walitembelea mradi wa ujenzi wa soko kuu la kisasa lililogharimu sh bilioni 17.6 na kituo cha mabasi cha msamvu kilichogharimu Sh.14 bilioni.
Akizunguimza katika majumuisho ya ziara hiyo Msukuma alisema kuwa pamoja na Halmashauri ya Wilaya Geita kuwa na mgodi mkubwa wa dhahabu lakini bado haijafanikiwa kujenga soko kubwa la kisasa na hata kituo cha mabasi cha kisasa hivyo ziara hiyo imewasaidia kujifunza mengi ikiwa ni pamoja na namna ya kubuni na kusimamia miradi mikubwa.
“Hii ziara imetusaidia kujifunza, tutakaporejea Geita tutaanza mchakamchaka wa kuanza kujenga soko kubwa kwa sababu uwezo tunao na hata eneo la kujenga tunalo,” alisema Msukuma.
Aidha aliiomba Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuwa tayari kuwapa wataalamu wa kuandika miradi mbalimbali kwa kuwa wamebaini Halmashauri hii inawataalamu wazuri na wenye ujuzi wa kutosha.
Hata hivyo Msukuma aliishauri Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuongeza vyanzo vya mapato katika kituo cha mabasi cha msamvu badala ya kutegemea chanzo kikubwa kimoja cha ushuru wa mabasi ambao kwa sasa uko kwenye mchakato wa kufanyiwa marekebisho ya kisheria baada ya kuonekana kuwa ni kero kwa wamiliki wa mabasi.
Katika ziara hiyo Mkuu huyo wa Wilaya ya Geita Josephat Maganga alisema kuwa katika ziara hiyo amejifunza namna viongozi wa Manispaa ya Morogoro walivyokuwa naumoja na wanavyoweza kutekeleza na kusimamia miradi kwa kushirikiana.
Alisema kuwa kama viongozi wa Halmashauri wangekuwa hawaelewani isingewezekana miradi hiyo kutekelezwa kwa kiwango na kwa wakati bila kuathiri wananchi.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Morogoro Pascal Kihanga alisema kuwa ujenzi wa soko hilo ulikuwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara kwenye soko la zamani.
Hata hivyo Kihanga alisema kuwa kutokana na viongozi wa Halmashauri kuwa na msimamo, ushirikiano walifanikiwa kuwahamisha wafanyabishara hao bila vurugu hata hivyo baada ya kukamilika wafanyabishara hao watapewa kipaumbele kwa kuwapatia vizimba vya kufanyia biashara kwa gharama nafuu itakayopangwa na Halmashauri.
Awali akitoa taarifa za miradi hiyo Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Michael Waluse alisema kuwa makusanyo ya mapato katika kituo cha mabasi msamvu kwa siku sio chini ya 3 milioni hata hivyo gharama za uendeshaji ikiwemo kulipa maji, umeme, usafi na misharaha ya watumishi wanaosimamia kituo hicho kwa mwezi sio chini ya Sh 25 milioni.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa