KAMATI ya Kudhibiti Virusi vya UKIMWI Manispaa ya Morogoro imesema kwa sasa watahakikisha wanaelekeza nguvu katika kuboresha mipango kazi ngazi ya Kata ili kudhibiti maambukizi mapya ya UKIMWI.
Kamati hiyo, imesema hayo Januari 23/2023, katika ziara ya kutembelea Kata ya Bigwa ambayo imeonekana kufanya vizuri katika maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Desemba 01/2022.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati , ambaye ni Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Sabasaba,Mhe. Mohamed Lukwele, amesema kumekuwa na kusuasua kwa maandalizi ya maadhimisho ya UKIMWI ngazi ya Kata, hivyo katika vipindi vijavyo watahakikisha wanafanya maboresho ya kuweka mikakati na mipango thabiti ya kuzipa nguvu kamati za Kata ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi.
" Leo tupo Kata ya Bigwa, wenzetu walifanya vizuri sana katika maadhimisho ya Siku ya UKIMWI ya mwaka 2022, Desemba ngazi ya Kata, kuna kila sababu ya kujifunza walifanikiwa vipi, niombe sana Kata nyingine wakati tunaelekea katika maadhimisho mengine ni vyema wakafika kujifunza lakini sisi kama Kamati tunaenda kuboresha na kuweka mipango yetu vizuri ya Kuongeza Bajeti , tunataka kamati zipewe umuhimu kulingana na majukumu wanayoyafanya ya kupunguza maambuziki mapya ya virusi vya UKIMWI" Amesema Mhe. Lukwele.
Pia, amewapongeza Viongozi Kata ya Bigwa kwa kufanikiwa kupunguza maambukizi ya watu wenye Virusi Vya UKIMWI, kwani takwimu imeonesha kutoka januari -Desemba , 2022 jumla ya waliopima walikuwa 195, ambapo katika idadi hiyo wanaume 87 na wanawake 108 katika Zahanati za Mgolole, Vituli na Misongeni.
Mbali na uhamasishaji wa watu kupima, mafanikio yao yalitokana na kuanzisha mradi wa TIMIZA MALENGO wenye lengo la mabinti wadogo kujiepusha kujiingiza katika masuala ya ngono wakiwa na umri madogo, ambapo katika mradi huo jumla ya Mabinti 133 walipatiwa elimu juu ya mradi huo.
Licha ya kuwa na mradi wa Timiza Malengo, Kata ya Bigwa walienda mbali zaidi na kuanzisha mradi ujulikano kama elimu bora kwa jamii ukiwa na lengo la kuielimisha jamii kuwa bora na kuwa na mtazamo chanya wa maisha.
Mwisho, Kamati hiyo imewataka wananchi kuwa na utaratibu wa kupima afya kwani kupima afya kuna faida ya Kujua afya zao na kuweza kupanga mipango yao , kunusuru afya ya mama na mtoto endapo ameathirika na kutoendelea kuambukiza na kupokea maambukizi mapya.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa