MANISPAA ya Morogoro ipo kwenye mpango wa kujenga Kituo cha Burudani ambacho kitakuwa na lengo la kuwakutanisha Wanamichezo na wasanii kwa pamoja .
Kauli hiyo ya ujenzi wa Kituo cha Burudani , imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro , Mhe. Bakari Msulwa, leo Oktoba 03, 2020 wakati wa kujumuika katika mazoezi ya pamoja na wadau wa michezo kwenye Viwanja vya Gymkhana Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Msulwa, amesema Ujenzi huo ni mpango ambao upo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
“”Nimeongea na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, amesema wao wana mpango huo, lakini ujenzi huo wa kituo cha burudani hautaishia katika michezo tu bali kituo hicho kitakuwa cha uwekezaji, tunataka wanamichezo wawe na kijiwe chao lakini sio kwa Manispaa ya Morogoro pekee bali hata Morogoro Vijijini lazima wawe na mpango huo huo wa kujenga Kituo cha Burudani, “”Amesema DC Msulwa.
Mbali na hayo,amewataka Wanamichezo kuadhimisha siku ya Mwalimu Nyerere kwa kujumika pamoja katika eneo la mradi wa Nyama Choma Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kusheherekea siku hiyo muhimu kwa pamoja ikiwamo kula na kunywa kwa ajili ya kujenga afya zaidi.
“”Tumekubaliana na Mkurugenzi hapa kwamba siku hiyo ndiyo inategemea mradi wa ujenzi wa nyama choma kuzinduliwa hivyo sisi wanamichezo kwa pamoja tutakutana hapo, tutakunywa supu na nyama choma, pamoja na vinywaji, baada ya hapo tunaongea na wadau wa michezo wakati tukiwa tumeshiba waone namna ya kuweza kutusaidia, kwahiyo tunataka siku hii iwe sherehe kubwa kwetu “”Ameongeza DC Msulwa.
Msulwa, amesema yote yanayofanyika ni kutengeneza mpango kazi utakaoweza kuwaunganisha wadau wote wa Michezo Wilaya ya Morogoro katika kuendeleza na kukuza vipaji vyao nap engine kuzalisha ajira kwa ajili ya maisha yao.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema siku ya Mwalimu nyerere atatoa ngómbe mmoja kwa wanamichezo .
“Niwaombe Wanamichezo tujitokeze kwa wingi, ngómbe mmoja siwezi kumla peke yangu, nawakaribisha sana katika mradi wetu mpya wa nyama choma nanenane , michezo ni afya na michezo ni ajira, Morogoro ya Viwango inawezekana tukishikana kwa pamoja”Amesema Lukuba.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Bi. Rehema Bwasi, amesema huu ni mwanzo , hivyo amewataka Wanamichezo kutokata tama kwani yapo mambo mazuri yanakuja.
“Nimefurahi kukutana nanyi tena katika juma hili, hii ni mara ya pili, tumpongeze sana Mkuu wetu wa Wilaya kwa kutuletea jambo hili katika kudumisha michezo katika Wilaya yetu ya Morogoro, niwaombe wanamichezo hiki ambacho Mkuu wetu wa Wilaya amekianzisha tuendelee kukidumisha, tunataka Morogoro ya Viwango iwe ya kweli na kurudisha heshima yetu katika Michezo “”Amesema Bwasi.
Katika hatua nyingine, Bwasi, amesema kuwa , muamko ni mzuri kwani kitendo cha Msanii mkubwa kama Rayvanny kuunga mkono suala la michezo na burudani inaonesha ni jinsi gani kampeni hiyo inakwenda kufanikiwa.
Katika hatua nyengine, Mbunge Mteule wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki , Mhe. Hamisi TaleTale maarufu kwa jina la Babu Tale , amewataka Wanamichezo kuendelea kutengeneza vipaji kwani Morogoro ni Mkoa ambao umejaliwa kuwa na vipaji vingi vya michezo.
“Niwaahidi tu wana Morogoro, tutashikana bega kwa bega kuhakikisha tunainua suala la michezo na sio katika michezo pekee bali hata kwenye Sekta ya elimu kama alivyozungumza Mkuu wa Wilaya”” Amesema Mhe. Tale.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa