MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe.Albert Msando, leo amewaongoza watumishi wa Ofisi ya Manispaa ya Morogoro kufanya Usafi wa mazingira nje ya eneo la Stendi ya Mabasi Msamvu ikiwa ni shamra shamra za sherehe ya Miaka ya 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo amesema umesaidia kuleta upendo na umoja miongoni mwa watumishi.
DC Msando, ameshiriki zoezi hilo la usafi (26.04.2022) katika maeneo ya nje ya Stendi ya Mabasi Msamvu huku akisisitiza kuwa watanzania wameendelea kuwa wamoja na wenye kuheshimiana hatua inayokuza utaifa.
“Leo ni siku muhimu kuona kama watumishi tukiwa na umoja na upendo kati yetu wa Bara na wenzetu wa Zanzibar kufuatia uwepo wa Muungano wa nchi zetu mbili. Tuuenzi Muungano wetu huu ili udumu kwa vizazi vingi zaidi vijavyo” Amesema DC Msando.
Aidha, DC Msando, ameiagiza Manispaa ya Morogoro kupanga vizuri Mji ikiwemo eneo hilo nje ya Stendi ya Mabasi Msamvu ili kuleta taswira nzuri ya mji tofauti na ilivyo sasa ambapo wafanyabiashara ndogondogo wamekuwa wakitumia maeneo ya barabara kupanga biashara zao kiholela.
Naye Katibu Tawala Wilaya ya Morogoro , Ruth John, amewapongeza watumishi wa umma waliopo Manispaa ya Morogoro pamoja na taasisi zilizopo Manispaa ikiwamo wadau wa mazingira na Viongozi mbalimbali wa Kata kwa kujitokeza kuadhimisha sherehe za Miaka 58 ya Muungano kwa kufanya Usafi hatua inayoongoza ushirikiano miongoni mwa watumishi hao.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Ally Machela, amesema tukio la usafi limepokelewa vizuri huku akiwapongeza Watumishi wa Manispaa ya Morogoro na wadau wa mazingira akisema kuwa kitendo cha kufanya usafi siku ya leo ni mwendelezo wa kuonesha umoja wa watanzania mahala pa kazi.
Machela, amewasihi wananchi wa Manispaa ya Morogoro kuendeleza mshikamano wa kidugu na wananchi wa Zanzibar ili kwa pamoja Tanzania ipige hatua zaidi ya kimaendeleo.
Watanzania leo wanaadhimisha sherehe za miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa