Wasilisho la mapitio ya Mpango wa Bajeti wa Manispaa ya Morogoro kwa mwaka wa fedha 2022/2023, 2023/2024, na Mpango wa Bajeti wa Mwaka 2024/2025 kwa Baraza la Wafanyakazi, limefanyika tarehe 08.02.2024 kwenye ukumbi wa mikutano wa Manispaa hiyo na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa Divisheni na Vitengo vya Manispaa, na wawakilishi na viongozi wa vyama vya wafanyakazi ngazi ya mkoa.
Mwenyekiti wa kikao hicho, ndugu Jeremiah Lubeleje, akimwakilisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, wakati wa ufunguzi wa kikao amesema, dhima ya kikao hicho ni kuangalia mtazamo wa bajeti katika kuhakikisha inawaletea manufaa wananchi wa Morogoro hivyo wajumbe watumie fursa hiyo kuonesha wajibu wao na kutoa ushauri utakoleta tija zaidi.
Katika hatua nyingine, ndugu Lubeleje amesema makisio ya mapato ya ndani ya manispaa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 yamepanda kwa asilimia 18.49 kwani katika bajeti inayoendelea hivi sasa makisio yalikuwa ni shilingi 13,185,280,000.00, na bajeti ya mwaka 2024/2025 makisio ni shilingi 15,622,877,022.05, shilingi 2,568,322,491.05 zikiwa ni mapato lindwa na shilingi 13,054,554,531.00 zikiwa ni mapato yasiyolindwa.
Ndugu Lubeleje ametaja miradi kipaumbele ya kimkakati ya Manispaa, ya mwaka 2024/2025 kuwa ni ujenzi wa maghala manne na eneo la kuegeshea malori katika eneo la SGR kata ya Kihonda.
“Miradi mingine ya kimkakati ambayo Manispaa inapanga kuitekeleza katika mwaka wa fedha 2024/2025 ni ujenzi wa ukumbi wa mikutano/sherehe na michezo ya watoto katika eneo la Manzese, ukumbi mkubwa, Hoteli ya nyota tano na nyumba maalum za kupangisha kata Mwembesongo, ujenzi wa kituo cha maegesho ya malori Nanenane kata ya Kichangani.
“Mingine ni ujenzi wa jengo la machinga kata ya Tungi, ujenzi wa shopping mall ya kisasa na Hoteli Msamvu kata ya Mafisa, ujenzi wa eneo la mapumziko na burudani kata ya Kihonda, ujenzi wa kituo cha michezo cha Uluguru, ujenzi wa Hoteli ya kisasa Kihonda mlimani, ujenzi wa nyumba za kupangisha, ujenzi wa machinjio ya kisasa kata ya mkundi, na ujenzi wa stendi ya mabasi ya ndani karibu na eneo la SGR Kihonda” alieleza kwa kina, Lubeleje.
Pia, ndugu Lubeleje amesema ili kupunguza adha ya usafiri na mazingira magumu kwa watumishi walioko maeneo ya mbembezoni sana, Manispaa kupitia fedha za mapato yake ya ndani inapanga kununua pikipiki kumi, sita kati ya hizo watakabidhiwa walimu wakuu wa shule za msingi Mbete (1), Sangasanga (2), Ujirani Mwema (2), na Mungi (1), na pikipiki nne watakabidhiwa watendaji wa kata za Bigwa (1), Mkundi (1), Mlimani (1), na Kauzeni (1).
Kwa upande wao wajumbe wa kikao hicho, wamemshukuru mkurugenzi wa Manispaa kwa kuwajali watumishi wa pembezoni na kupanga kuwanunulia pikipiki. Wamemwomba aendelee kuboresha mazingira ya watumishi wake hasa wa pembezoni kwa kukarabati nyumba zao ama kuwajengea mpya.
Aidha, wajumbe hao wamemshauri mkurugenzi wa Manispaa kuhakikisha wanafunzi wa shule za sekondari wanatumia viti na meza badala ya madwati kama inavyoshauriwa na wathibiti ubora wa elimu.
Wameshauri madwati yaliyopo kwenye baadhi ya shule za sekondari yapelekwe kwenye shule za msingi halafu fedha ambayo ingeelekezwa kwenye kuchonga madawati kwa shule za msingi itumike kuchonga meza na viti kwa shule za sekondari ambazo madawati yake yatachukuliwa.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa