Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amewataka Walimu wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari, kujitathimini na kuona Kama wanafaa kukaa Manispaa Morogoro.
Kauli hiyo ameitoa Januari 19, 2021 wakati wa ziara ya kikazi ya ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya Madarasa vilivyojengwa na Manispaa Morogoro na nguvu za wananchi kufuatia agizo la Serikali la kutaka wanafunzi wote kuingia darasani ifikapo Februari 28.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Kihanga, amesema kumekuwa na matokeo mabovu ambayo hayaridhishi jambo linalopelekea Manispaa kushika nafasi za nyuma huku ikiwa mjini.
Mhe. Kihanga, amesema kuwa, sasa ni wakati wa Waalimu hao kuanza kujitathimini upya kutokana na matokeo hayo.
" Nimeanza ziara ya kikazi ya kukagua ujenzi wa Shule na vyumba vya Madarasa, lakini matokeo bado hayaridhishi hususani katika upande wa Sekondari, tunashindwa hadi na wenzetu wa vijijini, sisi tuna kila kitu ila ni wapi tuna kwama? Hizi nafasi sio zetu, niwaombe Waalimu mjitathimini, Serikali inawekeza katika ujenzi na sisi tunataka matokeo mazuri, baada ya ujenzi wa madarasa tunahamia kwenu, kama umeshindwa kukaa Manispaa ondoka kabisa, tunataka matokeo mazuri tufanane na hadhi yetu ya Manispaa" Alisema Mhe.Kihanga.
Aidha aliwataka Waalimu wakuu wanapokaa katika vikao vyao wamualike ili wazungumze kwa pamoja na kuona changamoto ambazo zipo na kuzitatua. Suala la Waalimu amesema kuwa mpango uliopo kwa sasa ni kuongeza Waalimu wa Sayansi ambao ndio changamoto kwa Sasa. Kuhusu Ujenzi wa Shule ya Msingi Konga, amempongeza Sana Mkurugenzi Manispaa Morogoro Sheilla Lukuba, kwa jitihada za kupambania Sekta ya elimu, kwani Sasa amekuwa akitoa fedha nyingi katika kata kwa ajili ya maendeleo mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu.
" Mkurugenzi wetu anajitahidi Sana , tumtumie vizuri, anahangaika Sana, sisi hatuhitaji kubweteka, tufanye kazi, haya matokeo yanatuumiza Sana, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi wote tunaumia, huu ni muda wa kujipanga sasa tutoke hapa tulipo twende mbele"Aliongeza Mhe. Kihanga.
Mwisho , amesema kuwa ziara hizo zitakuwa endelevu, lakini kwanza ameanza katika Shule za Sekondari baada ya hapo atahamia Shule za Msingi. Miongoni mwa Shule alizoanza nazo ziara ni pamoja na Shule ya Msingi Konga Kata ya Mzinga, Shule ya Sekondari Kihonda Kata ya Mazimbu, Shule ya Sekondari Sumaye Kata ya Bigwa na Shule ya Sekondari Lupanga Kata ya Kilakala.
Naye Diwani wa Kata ya Kilakala, Mhe. Marco Kanga, amemshukuru, Mstahiki Meya kwa ziara hiyo huku akimuahidi kumpa ushirikiano na kuhakikisha anafuatilia kwa ukaribu maswala ya elimu katika Kata hiyo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa