MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Mazimbu, Mhe. Pascal Kihanga, amewataka Wananchi kujitokeza kwa wingi katika Awamu ya pili ya Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuwahimiza Wananchi waliotimiza miaka 18 na wale ambao walishajiandikisha awamu ya kwanza wajitokeze kwa wingi kuhakiki taarifa zao ili kutimiza haki zao za kuwachagua viongozi wanaowataka katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka 2020.
Kihanga , ameyasema hayo leo Mei 2, 2020 Kwenye Ofisi ya Kata ya Mazimbu wakati alipokwenda kuhakiki taarifa zake kwenye Kituo alichojiandikishia kilichopo Mtaa wa Modeco 'B' .
Aidha, amewata Madiwani wote kutumia fursa hii kuwaagiza Wenye Viti wao wapitie nyumba hadi nyumba kuwahimiza Wananchi wao kwenda kuhakiki taarifa zao kwani muda uliopo sio rafiki.
“Tuna muda mchache sana, leo Jumamosi na Jumapili ni siku za mapumziko , kwa Wafanya kazi na wale watumishi wazitumie siku hizi kikamilifu kuhakiki taarifa zao ili itakapoanza Jumatatu siku za kazi basi waendelee na majukumu yao mingine , muda sio rafiki kwentu siku hizi 3 sio nyingi sana, niwaombe tusidharau lazima mtambue kwamba zoezi hili ni muhimu sana , mimi nimehakiki taarifa zangu lakini Picha haipo kwahiyo ikanibidi nikapige picha upya na kupewa kitambulisho changu kipya, ukidharau unaweza ukajikuta unapoteza sifa za mpiga kura katika uchaguzi” Amesema Kihanga.
“Zoezi hili limeanza lazima Wananchi walipe kipaumbele na kuacha dharau, napenda kuwaomba Wananchi wa Manispaa ya Morogoro kwenye Kata zote 29, wajitokeze kwa wingi kwani zoezi hili linahusika na uandikishaji wa wapiga kura wapya wenye sifa ili waweze kupata fursa za kushiriki kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka 2020” Amesisitiza Kihanga.
Pia amewaomba wale wananchi waliohama kutoka eneo moja kwenda jengine waende katika Vituo walivyopo kwa sasa ili waweze kuhamisha taarifa zao katika Daftari la wapiga kura ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuwachagua Viongozi katika uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo, amesema wapo wale ambao wamefikisha umri wa miaka 18 au wanafikisha mwaka huu kabla ya Mwezi Oktoba, waende katika Vituo ili waweze kurekebisha taarifa zao na wale ambao wamehama Mkoa, eneo nje ya Kata pamoja na kutoka Jimbo moja kwenda jengine wote wanatakiwa wakahakikihi taarifa na kuweza kuhamisha taarifa zao.
Hata hivyo ameendelea kutoa rai kwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro kuendelea kufuata ushauri wa Wataalamu wa Afya katika kujikinga na Ugonjwa wa Corona ikiwemo kunawa Maji tiririka na sabuni, kutumia Vitakasa mikono ( Sanitizer), pamoja na kuepuka msongamano isiyo ya lazima na kukaa nyumbani kama mtu hana sababu ya Msingi ya kutoka
Naye , Afisa Mwandikishaji Msaidizi wa Jimbo Morogoro Mjini, Waziri Kombo , amesema bado hajaridhishwa na Mwitiko wa watu , hivyo amewataka Wananchi kuacha kupuuzia swala hilo kwani wasipofanya hivyo kuna hatihati ya wale ambao taarifa zao hazitakuwa sahihi au kutoonekana kwa picha zao wakapoteza sifa ya kupiga kura.
Katika hatua nyenge, Kombo,amesema kumekuwa na changamoto ya kutoonekana kwa picha za watu katika Vituo, hivyo wananchi wanatakiwa watambue uhakiki ni jambo muhimu sana ili waweze kuwa na sifa za kupiga kura.
“Serikali inajicho pana , ndio maana kuna zoezi la uhakiki, ukiangalia changamoto kubwa ambayo nimeiona ni kutokuonekana kwa picha za watu katika majina yao waliyojiandikisha mwanzo, niwaombe wale ambao wanashida hiyo wakapige picha upya kwenye vituo vilivyowekwa, na uhakiki pia ni muhimu ili changamoto hii iweze kupatiwa ufumbuzi , kama tutadharau ujue kabisa utajipotezea sifa ya kuwa mpiga kura na kukosa haki yako ya msingi na ya kikatiba” Amesema Kombo.
Kombo, amewataka waandikishaji kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo la Uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili na kutekeleza zoezi hilo kwa kwa umakini na ufanisi pamoja na utunzaji wa vifaa vyote vitakavyohusika katika zoezi hilo.
Amesema matarajio yake ni kuona zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga Kura linafanikiwa kwa kiwango kikubwa ili kuwa na taarifa sahihi za wapiga Kura.
Pia amesema njia mbadala zitakazotumika katika uhakiki wa daftari ni kama zifuatazo;
I. Bonyeza *152*00#ok
II. Chagua Namba 9 ambayo ni Uchaguzi Mkuu
III. Chagua tena Namba 1 ambayo ni Uhakiki Taarifa za Mpiga Kura
IV. Baada ya hapo unatakiwa kuingiza Namba ya Mpiga Kura (Utaweka Namba peke yake bila ya herufi (T) wala , Dash (-)
Kwa upande wa Afisa Mtendaji wa Kata ya Mazimbu, Bi. Prisca Mawala, amesema kwa upande wa Kata ya Mazimbu wamewahamasiha sana Wananchi kwa kutumia gari la mapatangazo hivyo matarajio yake hizi siku mbili mahudhurio yataongezeka huku akiomba uhamasishaji zaidi kupitia kwa Wenyeviti wa Mitaa na wajumbe wao.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa