Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imetoa mikopo ya kiasi cha Sh milioni 133.5 kwa vikundi 45 vya wanawake ,vijana na watu wenye ulemavu katika mwaka wa fedha 2018/2019 kwa lengo la kuongeza mitaji yao ili kuwawezesha kuzalisha kwa wingi bidhaa mbalimbali na kuongeza vipato vyao kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi katika familia zao.
Ofisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Morogoro, Enedy Mwanakatwe alisema hayo katika risala ya wanawake wa Manispaa ya Morogoro kwa mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Morogoro , Regina Chonjo katika kilele cha maadhimisho ya wanawake Duniani yaliyofanyika ki wilaya Machi 8 kwenye uwanja wa Jamhuri wa mjini hapa.
Mwanakatwe alisema , kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019 , halmashauri iliweza kutoa mkopo wenye thamani ya Sh milioni 66 kwa vikundi 22 vya wanawake na kiasi kingine cha Sh milioni 37 kwa vikundi 12 vya vijana.
Alisema ,halmashauri imezingatia agizo la Serikali la kutenga asilimia mbili ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya watu wenye ulemavu na jumla ya Sh milioni 30.5 zimetolewa kwa vikundi 11.
Pia alisema ,kupitia Mfuko wa Jimbo umewezesha Jukwaa la Wanawake kiuchunmi (JUWAKIMAMO), vyerehani 17 na mashine za over lock mbili zenye thamani ya Sh milioni tano ambazo zilikabidhiwa na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood , mwishoni mwa mwaka jana .
“ Matarajio ya mradi huu ni kufungua chuo kwa ajili ya mafunzo ya ushonaji kwa wanawake wa Manispaa ya Morogoro wakiwemo vijana wa kike na wakiume wenye uhitaji” alisema Mwanakatwe.
Pamoja na hayo halmashauri ya Manispaa kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imefanikiwa kusajili vikundi 167 tangu Januari mwaka 2018 hadi kufikia Februari 2019 .
Naye Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) , Wilaya ya Morogoro mjini Kichama, Sofia Kibaba ,aliishauri halmashauri hiyo kuendelea kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya makundi hayo na hasa la watu wenye ulemavu ambao wamesahauliwa zaidi na kupatiwa elimu ya masaada wa kisheria kwa wanawake na makundi hayo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Chonjo aliwataka walionufaika na mikopo waitumie kulingana na mahitaji yaliyokusudiwa kwa kuendeleza vikundi vyao kiuchumi.
Pamoja na hayo aliwataka wazazi na walezi wawahamasishe wanafunzi wa kike kupenda masomo ya sayansi ili taifa liweze kuwapata wataalamu wengi wanawake kwenye nyanja za madaktari na wahandisi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa