MKURUGENZI wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema tayari Manispaa ya Morogoro imeshachukua hatua za haraka za kutekeleza agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Mjaliwa , la ujenzi wa Makaburi pamoja na mnara kwa walifariki na ajali ya moto.
Kauli hiyo ameitoa leo Mei 14, 2020 ,mara baada ya kuzuru katika makaburi hayo kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya ujenzi ,kufuatia kauli ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania , Mhe. Kassim Majaliwa kutaka makaburi na mnara yajengwe ili kuendelea kuwaenzi marahemu.
Aidha, Lukuba, amemuagiza Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro, Juma Gwisu kwenda na kasi zaidi ya kukamilisha ujenzi wa Makaburi hayo pamoja na mnara.
“Huu ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu , Mhe. Kassim Majaliwa, alivyokuja Manispaa yetu kutembelea makaburi kwa mara ya kwanza ambapo aliagiza tuboreshe na tuanze ujenzi wa makaburi pamoja na mnara mkubwa ambao utakuwa na majina yote ya marehemu kama moja ya njia za kuwaenzi, uzio tayari tumemaliza kujenga, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro , Eng. Emmanuel Kalobelo ameshatupatia fedha kupitia mfuko wa maafa zilizokusanywa kwa ajili ya marehemu hawa, kwahiyo ujenzi umeanza , kikubwa niwaombe ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu wazidishe maombi wanapokwenda katika nyumba za ibada" Amesema Lukuba.
Hata hivyo, amesema katika ujenzi huo , litatengwa eneo rasmi litakalo tumika kwa ajili kufanyia sala na maombi kwa marehemu wote .
“Licha ya kuboresha makaburi lakini kutokana na uzito wa eneno, tumeona tutenge eneo la kufanyia sala na maombi, eneo hili dini zote watakaa na kila mtu ataomba kwa mujibu wa taratibu za dini yake , nizidi kuwaomba ndugu wa marehemu tuwe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu, kuondokewa na ndugu zetu kusitufanye turudi nyuma kikubwa ni kuwaombea na kuendelea kufanya kazi kwa ajili ya familia zetu na maendeleo yetu tunatambua marehemu wameacha watoto, familia na tegemezi lakini yote ni mipango ya Mungu kila mtu atapitia njia hiyo muda na wakati ambao Mwenyezi Mungu atamuhitaji” Ameongeza Lukuba.
Lukuba, amesema mara baada ya ujenzi huo kukamilika , kutakuwa na utaratibu wa maadhimisho ya kuwakumbuka na kuwaombea marehemu wote kila mwezi wa 8, tarehe 10 ambapo ndipo tukio la ajali ya moto lilitokea.
Ikumbukwe kuwa, mkasa huo ulitokea majira ya saa mbili asubuhi ya Jumamosi baada ya lori lilibeba shehena ya petroli kuanguka katika mji wa Morogoro, na watu kuanza kuchota mafuta yaliyomwagika kisha mlipuko mkubwa kutokea.
Naye Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro, Juma Gwisu, amesema ujenzi wote wa makaburi, fensi pamoja na mnara utagharimu kiasi cha shilingi Milioni 35 na mradi huo unatarajiwa kumalizika Juni 10,2020.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa