Wazazi na walezi wa watoto wenye maradhi ya Vichwa vikubwa na mgongo wazi mkoani Morogoro wameshauriwa kutowaficha ndani watoto hao na badala yake kuwapeleka mapema Hospitali na Vituo vya Afya ili kupatiwa matibabu stahiki kwa ajili ya kuwaondolea matatizo.
Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo alitoa ushauri huo ,hivi karibuni katika hotuba iliyosomwa na Katibu tawala msaidizi wa wilaya ya Morogoro , Yahya Nania ,wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu yenye lengo la kutoa elimu namna ya kuwahudumia watoto wenye maradhi hayo.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na Chama cha wenye watu walemavu wa vichwa vikubwa na mgongo wazi Tanzania (ASBATH) mkoa wa Morogoro na kufanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Alisema , tatizo hilo linaweza kuepukika endapo akina mama wajawazito watafika kwa wakati katika kliniki kama inavyosahuriwa na madaktari na kupatiwa dawa ya kinga ya tatizo hilo.
“Tatizo hili linaweza kuzuilika kwa mama mjamzito kama atafika kliniki mapema na kupatiwa dawa ya foric Acid kwa kuwa tatizo hili , huanza kwa mama mjamzito kuanzia siku ya 14 hadi 21, hivyo ni muhimu kufika kliniki mapema.” alisema Nania.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro , Dk Frank Jacob alisema kuwa, wanawake wajawazito wakifika mapema hospitalini na vituo vya Afya kutasaidia kupata matibabu na ushauri wa kina na hivyo kupunguza au kutokomeza kabisa tatizo la watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.
“Watoto hawa wanaweza kutibiwa matatizo haya na kuendelea na shughuli zao kama kawaida endapo watafikishwa mapema Hospitalini kupatiwa tiba , hivyo hakuna haja ya kuwaficha majumbani watoto hawa au kuona tatizo hilo ni laana.” alisema Dk Jacob .
Naye Mwenyekiti Asbath Tawi la mkoa wa Morogoro Colimba Mbiki alisema , tawi lilianzishwa mwaka 2012 na watoto wanne na hadi kimeweza kusaidia watoto 167 kupata tiba kati yao 70 ni wavulana na 63 wasichana , licha ya juhudi hizo lakini watoto 44 wamefariki kwa magonjwa mbalimbali wakiwa na umri wa miaka mitano hadi 10.
Mbiki alisema , chama wanakabiliwa na changamoto kubwa ya usafiri ili kuwafikia walengwa , umbali mrefu wa kwenda hospitali na vituo vya Afya .
Hivyo aliiomba Serikali kuwasaidia kupatiwa huduma ya matibabu katika hospitali za rufaa katika mikoa na vifaa tiba zikiwemo pampasi , mipira ya mkojo , viti vya magurudumu kwa njia ya msamaha.
“ Wazazi wengi wanakosa uelewa na kukata tamaa kuona hali za watoto wao wakidhani wamelogwa au ni mikosi anapopata mtoto mwenye ulemavu huu , kwa hiyo ni kazi kwa viongozi kwenda kutoa elimu ili hatimaye kuwapekela hospitalini “ alisema Mbiki.
Kwa upande wake Mratibu wa Asbath Taifa , Hidaya Alawi ,pamoja na mambo mengine alikabidhi viti vya magurudumu vitano vikiwemo vyenye sehemu ya kujisaidia haja kubwa na ndogo .
Vifaa vingine ni vyandarua jozi 50 , sabuni na sukari ambavyo vimetolewa na Serikali kupita Hospitali ya Muhimbili kitengo cha MOI chini ya Ustawi wa jamii katika hospitali hiyo kwa kushirikiana na chama hicho kwa lengo la kusaidia jamii hiyo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa