NAIBU Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Mohamed Lukwele, amefungua Semina ya mafunzo ya Mfumo wa Anwani ya Makazi kwa mikoa 13 na Halamshauri 23 hapa nchini.
Mafunzo hayo yamefunguliwa leo Desemba 18/2021 katika Ukumbi wa CCT uliopo Kata ya Kilakala Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza juu ya mafunzo hayo, Mhe. Lukwele, amesema kuwa utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi unalenga kuharakisha na kurahisisha upatikanaji, utoaji na upelekaji wa huduma ama bidhaa hadi mahali stahiki.
Mhe. Lukwele, amesema kuwa Mfumo wa Anwani za Makazi, unawezesha kufanyika kwa biashara mtandao.
“ Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila Mwananchi, Ofisi ama eneo la biashara linakuwa na Anwani ya Makazi, kwahiyo ili kurahishsa Mfumo huo ni vyema kila Halmashauri ikaweka msukumo katika kujenga uwezo kwa watendaji na wataalamu wa Kata na Mitaa/ Vijiji ikiwa ni pamoja na uwezo katika matumizi ya Programu Tumizi ya Mfumo” Amesema Mhe. Lukwele.
Aidha, amewataka Watendaji wa Vijiji/Mitaa watumike katika kukusanya taarifa za Anwani za Makazi na kutoa Anwani husika kwa Wananchi kwa kutumia Programu Tumizi.
Pia, amewataka Wadau wakiwemo Wananchi wahamasishwe kujiwekea miundombinu wa mfumo katika maeneo yao ya Makazi, Ofisi ama eneo la biashara.
Aidha, ameipongeza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari kwa kujenga uwelewa kwa Viongozi kuanzia Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi wa Halamshauri zote nchini pamoja na Mameya/ Wenyeviti wa Halamshauri huku akisema hatua hiyo ya kushirikisha kada zote itaharakisha utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi.
Mwisho, amesema kutokana na umuhimu wa Anwani za Makazi katika Nyanja zote za Kiuchumi na Kijamii, ni vyema suala la Anwani za Makazi iwe ajenda ya kudumu katika vikao vya ngazi zote ili kuchochea utekelezaji na matumizi ya mfumo.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Mawasiliano Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Nchwekeleza, amesema kuwa amesema Mfumo wa Anwani za Makazi utaisaidia Serikali kupanga mipango ya Maendeleo, kuimarisha usalama, kuongeza ajira na Mapato ya Serikali.
Eng. Nchwekeleza, amesema mfumo huo utaendana na programu tumizi (mobile application) ya mfumo wa anwani za makazi ambayo itakayorahisisha matumizi na utekelezaji wa mfumo kwa kuzingatia kwamba itatumika katika kukusanya taarifa za Barabara, wakazi, makazi pamoja na kutoa anwani za makazi ya wananchi,kaya, ofisi na eneo la biashara.
“Dhamira ya Wizara kila mwananchi anakuwa na anwani yake ya makazi katika eneo analoishi, eneo la ajira au eneo la biashara, nitoe wito kwa watendaji, viongozi na wataalamu hususani wa kata na mitaa wajengewe uwezo wa kutosha ili waweze kuwa na uelewa wa pamoja,waweze kuratibu, kusimamia na kutekeleza mfumo huu” Amesema Eng. Nchwekeleza,
Aidha,amesema kwa kutumia utaratibu huu wa anwani za makazi, mpango shirikishi ulioandaliwa baina ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar wa kutekeleza zoezi hili utasaidia sensa ya watu na makazi ya mwakani kufanyika vizuri sana kwa sababu pia itaonyesha wananchi wanapokaa na wanafanya kazi gani.
Miongoni mwa Mikoa 10 inayo jumuisha Halmashauri 23 iliyoshiriki katika Mafunzo hayo ni pamoja na Jiji la Dar Es Salaam, Mwanza , Mbeya, Arusha, Tanga, Dodoma na Mikoa ya Morogoro,Mara, Kagera, Pwani , Iringa, Shinyanga na Geita.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa