MKUU wa mkoa wa Morogoro Mhe.Fatma Mwassa ameitaka jamii kujenga mifumo bora ya malezi katika familia zao.
Kauli hiyo ameitoa Mei 15/2023. katika maadhimisho ya siku ya familia duniani yaliyofanyika katika uwanja wa mpira wa miguu shule ya Msingi Mwere Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Jamii iliyojitokeza katika Maadhimisho hayo, amewataka Viongozi katika ngazi mbalimbali wahamasishe na kuhimiza watumishi wote kuona njia bora za kugawa muda wa kazi na muda wa kushughulikia familia zao ili kujenga maadili na maendeleo ya familia.
"Nitoe rai kwa jamii kuhakikisha kuwa kila mwanafamilia pamoja na utafutaji wake anakua balozi mzuri wa kufikisha ujumbe kwa watoto ikiwemo kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali kama vile ubakaji,ulawiti pamoja na aina mbalimbali za unyanyasaji wa kijinsia ikiwa na lengo la kujenga misingi mizuri ya maadili katika familia "Amesema RC Mwassa.
Aidha, RC Mwassa, amesema ni matumaini yake kupitia maadhimisho hayo ya familia zitakumbushwa wajibu na mchango wao katika maendeleo ya familia zao, jamii na Taifa kwa ujumla.
Pia amevitaka vyombo vya habari kutumia peni na dafatari vizuri kuelezea dhumuni la siku hii na kuandaa vipindi vyenye kuelimisha jamii masuala mbalimbali ya ukatili.
Hata hivyo, RC Mwassa, ametoa wito kwa viongozi wa dini kuhubiri na kuwaidhi kwa kukemea na kuonya madhara ya unyanyasajiwa kijinsia katika maeneo yao ya kuabudu.
Ikumbukwe kuwa Siku ya familia Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Mei na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ambapo maadhimisho hayo yanatokana na tamko la Baraza la Umoja wa Mataifa Na. 47/257 la tarehe 20 Septemba 1993, linaloadhinisha kuwa na Siku maalum kwa ajili ya Familia huku Tanzania ikiwa ni moja ya wananchama wa Umoja wa Mataifa hivyo huungana na nchi nyingine kila mwaka kuadhimisha. "KAULI MBIU 2023 IMARISHA MAADILI NA UPENDO KWA FAMILIA IMARA"
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa